Suleiman Msuya
JUMLA ya watahiniwa 408,442 wamesajiliwa kufanya mtihani
wa kidato cha nne mwaka huu unaoanza leo, imeelezwa.
Kati yao, 355,995 ni wa shule na 52,447 ni wa kujitegemea
ikilinganishwa na watahiniwa 448,382 wa shule wa mwaka jana.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA),
Dk Charles Msonde alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari
jana Dar es Salaam.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule 355,995 wavulana ni
173,423 sawa na asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa na asilimia 51.28, huku
wasioona 59 na wenye uoni hafifu wakiwa 283.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa 52,447 wa kujitegemea,
25,529 sawa na asilimia 48.68 ni wavulana na 26,918 sawa na asilimia 51.32 ni
wasichana huku wasioona wakiwa saba; wanawake watatu na wavulana wanne; mwaka
jana walikuwa 54,317.
Alisema katika Mtihani wa Maarifa (QT), jumla ya
watahiniwa 20,634 walisajiliwa kufanya mtihani huo mwaka huu, wanaume ni 7,819
sawa na asilimia 37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11; mwaka jana
walikuwa 19,547.
“Watahiniwa nchi nzima naamini wameajiandaa vya kutosha,
hivyo ni vema wakazingatia misingi ya taratibu za mitihani kwani hatutavumilia
mtu atakayejaribu kudanganya,” alisema.
Alisema maandalizi kwa ajili ya mitihani hiyo
yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuisambaza mitihani pamoja na vijitabu vya
kujibia na nyaraka zote muhimu katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.
Umuhimu
Akizungumzia umuhimu wa mtihani huo, Dk Msonde alisema ni
kupima uwezo na uelewa wa mwanafunzi katika aliyojifunza kwa miaka minne.
Dk Msonde alisema matokeo ya mtihani huo yatatumika
kuchagua wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na fani mbalimbali za utaalamu
wa kazi kama vile afya, ualimu, kilimo, ufundi na nyinginezo.
Katibu Mtendaji huyo alisema mikakati yao ni kuhakikisha
wanakuwa na taarifa ambazo zitaonesha idadi ya wanafunzi walioanza darasa la
kwanza hadi la saba.
0 comments:
Post a Comment