Peter Mziray
|
BARAZA la Vyama vya Siasa nchini
limesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Serikali vina dhamira ya kuua
vyama vya siasa nchini.
Kauli hiyo ya Baraza imetolewa na
Mwenyekiti wake, Peter Mziray wakati akizungumza na JAMBO LEO jana kwa njia ya
simu siku chache baada ya kurejea nchini.
Mziray alisema kwa muda mrefu Baraza
limekuwa likiomba vikao vya wajumbe wake ili kuzungumza na kutatua changamoto
linazokabiliana nazo za kisiasa ila ofisi hiyo imeshindwa kuviwezesha.
Alisema hali ya kisiasa nchini si nzuri,
hivyo wajumbe wamekuwa wakihoji sababu ya kutokutana hali ambayo inampa wakati
mgumu akiwa Mwenyekiti.
“Serikali hii haitaki vyama vya siasa
kabisa, kwani kila tukifanya jitihada za kutukutanisha tunakwama na ninachoona
hapa kikwazo ni Mwenyekiti,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema ni jambo la
kushangaza kuona Rais John Magufuli anaonekana kuchukia vyama vya siasa huku
akitokana na vyama hivyo hivyo.
Mziray alisema iwapo hakutakuwa na
uwezekano wa wao kukutana wataandaa mkutano hata chini ya mwembe kwani bila
vyama kukukutana vinaweza kufa.
Alisema kitendo cha vyama kutofanya
mikutano ni kuua vyama vikubwa kama CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, hivyo
kuitaka Serikali kuachana na utaratibu huo wa kuzuia siasa.
Mziray alisema wakati ofisi hiyo
ikishindwa kuwapa fedha za kuandaa vikao vya wajumbe, imetoa barua ya kutaarifu
vyama vya siasa kuhusu nia yake ya kufanya ziara za kukagua vyama ngazi za
wilaya.
Akizungumzia hali hiyo, Msajili Msaidizi
wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema malalamiko hayo hayana ukweli
na kuweka bayana kuwa Baraza hilo limekuwa likikutana kupitia Kamati ya
Uongozi.
“Kama sijakosea, wakati wa harakati za
Umoja kwa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) Kamati ya Uongozi ilikutana, hivyo
si sahihi kusema hatujafanya vikao labda aseme lingine,” alisema.
Nyahoza alisema sababu ya kutoitisha
vikao vingine kwa siku za karibuni, Baraza hilo linatarajia kufikia kikomo
mwezi huu hivyo watakutana kujadiliana na kufanya uchaguzi wa uongozi mpya.
Alisema ofisi yake haina nia yoyote ovu
ya kuua vyama vya siasa kwa kuwa vyama hivyo vipo kwa mujibu wa Katiba na
sheria.
0 comments:
Post a Comment