MWAKA MMOJA IKULU:
*Ajizatiti
kuyakabili licha ya ahadi zilizomtangulia
*Atoa maagizo ya
‘kutafuna mifupa’ iliyoshindikana
Fidelis Butahe na Suleiman Msuya
HATUA ya Rais John Magufuli kumteua Mkuu wa Majeshi
mstaafu Jenerali George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za
Taifa (Tanapa), umeelezwa kwamba unaweza kuwa ishara ya kufungua ukurasa mpya
wa kuanza kupambana na mambo matano makubwa ya ufisadi lakini pia yenye maslahi
kwa Taifa.
Uchambuzi wa JAMBO LEO na maoni ya wachambuzi unabainisha
kuwa mambo hayo matano ambayo Rais Magufuli anatajwa kuyageukia ili kuyakabili
na kuyamaliza, ni pamoja na vita dhidi ya ujangili, mikataba mibovu na usiri
wao, dawa za kulevya, migogoro ya ardhi na kumaliza au kuanza upya mchakato wa Katiba
mpya.
Kauli ya hivi karibuni ya Rais Magufuli kumtoa hofu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akimtaka
kukamata majangili bila kujali dini, kabila wala cheo cha mtu ni ishara ya
kufungua ukurasa huo wa mapambano ambayo wachambuzi wanasema yanaweza kufanikiwa.
Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais Magufuli
amefanya mambo mbalimbali, ikiwamo kuvunja bodi za taasisi na mashirika ya
Serikali, kuwahamisha kazi na kutengua uteuzi wa vigogo mbalimbali, akiwamo aliyekuwa
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, jambo ambalo
linahusishwa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa awali dhidi ya ujangili nchini.
Wadau
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
(MNMA), Mabuba Kisena alisema ni mapema kutafsiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa
kushughulikia maeneo hayo na kwamba anaamini sasa anatengeneza mfumo wa
uwajibikaji.
Kisena alisema changamoto ambazo zimekuwa zikilikumba
Taifa katika ujangili, dawa za kulevya na mikataba, asilimia kubwa zinatokana
na mfumo uliokuwapo kuruhusu mazingira ya rushwa.
”Mimi naamini akifanikiwa kunyoosha kwenye uwajibikaji wa
watumishi kuanzia ngazi ya chini hadi juu, hayo yote ambayo yanaonekana
kutoguswa yataguswa na matokeo chanya yataonekana,” alisema
Mhadhiri Paul Mtasigazya wa chuo hicho pia, alisema hatima
ya yote yanayolalamikiwa ni Katiba mpya na ukweli kwamba Rais Magufuli
amefanikiwa kufanya mambo yanayotia moyo.
“Naamini kuwa Katiba inaweza kujibu maswali yote ambayo
yapo kwa sasa kwani kuwepo kwa siasa, biashara na mgongano wa kimaslahi ni
mambo ambayo yatajibiwa na Katiba mpya,” alisema.
Mtasigazya alisema katika kipindi hiki ambacho bado
Katiba haijapatikana, ni jukumu la Rais kufanya kazi kama timu, kwani kinyume
cha hapo hawezi kufikia mwafaka wa anachokitaka.
Alisema bado kuna changamoto ya watumishi wa umma kumwelewa,
hivyo wanapaswa kupewa mafunzo ili kuendana na kasi yake.
Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Daniel Zenda alisema masuala ya dawa za kulevya na ujangili ni
mtandao mkubwa unaohitaji mipango iliyokamilika kuidhibiti.
Alisema pia mikataba ya nchi inapaswa kuchunguzwa kwa
umakini kwani kinyume na hivyo, Serikali inaweza kuingia kwenye hasara kubwa.
“Nadhani unaona katika viwanja vya ndege na mipaka hali
ilikuwa mbaya ila baada ya kuweka mashine hali imeanza kurekebika, hivyo Rais
anapambana kisayansi,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Zanzibar,
Mussa Kombo Mussa alisema hatima ya yote yanayolalamikiwa muarobaini wake ni
Katiba Iliyopendekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Alisema Katiba hiyo iliweza kuanisha kila kitu hivyo
itamrahisishia Rais kufanikisha malengo yake kirahisi bila kutumia nguvu.
Ujangili
Rais alimtoa hofu Jenerali Milanzi baada ya kutembelea
ghala la Wizara hiyo na kujionea vifaa vilivyokamatwa, yakiwamo meno ya tembo
50.
Kitendo cha Jenerali huyo kuulizwa na Rais kama ana hofu
yoyote na kujibu kuwa chini ya ‘sapoti’ yake hana hofu yoyote ni ishara kuwa Dk
Magufuli amejitosa kupambana na mtandao huo.
Lakini uteuzi wa Jenerali Waitara ndio unaonesha dhahiri
jinsi alivyodhamiria kupambana na vigogo wa ujangili ambao wametamba kwa muda
mrefu licha ya juhudi kadhaa zilizofanyika.
Februari 14 mwaka jana, Rais mstaafu Jakaya Kikwete
wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC alisema Serikali imebaini mtandao
wa ujangili unaojumuisha watu 40, akiwamo tajiri maarufu mkoani Arusha, lakini
haukuwekwa wazi kipindi hicho.
Mihadarati
Mtandao mwingine ambao umekuwa mgumu kufichuliwa ni wa
dawa za kulevya, licha ya viongozi kueleza mara kadhaa kuwa wanawafahamu
wahusika.
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa njia ya kupitisha au
kituo cha dawa za kulevya aina ya heroin, cocain, mandrax na morphine na mara
kadhaa mizigo imekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na
kiwango kikubwa kukamatwa nje ya nchi baada ya kupita kwenye uwanja huo.
Licha ya watu wa kada mbalimbali kutaka Serikali kufichua
mtandao huo unaodaiwa kuhusisha hata vigogo serikalini, wafanyabiashara wakubwa
na vigogo wa Polisi, lakini mpaka sasa wanaokamatwa ni wanaobeba na si wenye mitandao.
Katiba Mpya
Kitendawili kingine kinachosubiri kuteguliwa na Rais
Magufuli ni Katiba Mpya. Rais tayari ameshatamka wazi kuwa mchakato huo
utaendelea pale ulipoishia.
Mapendekezo yaliyotolewa hivi karibuni na wadau, ni
mchakato huo kuanzia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba huku
wakipinga Katiba Inayopendekezwa kwa maelezo kuwa iliacha maoni ya msingi ya
wananchi.
Ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uweze kuendelea,
Serikali italazimika kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni,
ili kuibadili iendane na wakati wa sasa kwa ajili ya kuendelea na mchakato huo
ulioishia katika upigaji kura ya maoni.
Migogoro ya Ardhi
Migogoro ya ardhi nchini imekuwa chanzo cha mapigano
baina ya wakulima na wafugaji na kupoteza uhai wa watu na mifugo, migogoro ya
wananchi na wawekezaji na uvamizi wa maeneo yasiyoruhusiwa kwa ujenzi,
yanaonekana kutopatiwa ufumbuzi.
Mara kadhaa imeelezwa matatizo hayo yanatokana na ardhi
kutopimwa na kugawanywa vizuri, lakini bado hayajatatuliwa.
Maeneo yaliyokithiri kwa migogoro hiyo ni mikoa ya
Manyara, Arusha na Morogoro ambako mapigano kati ya wakulima na wafugaji
hutokea mara kwa mara.
Mikataba mibovu
Licha ya wananchi kupiga kelele kuhusu mikataba mibovu na
usiri wao, bado suala hilo limekuwa kama barafu iliyowekwa juani.
Hadi sasa, hakuna kiongozi aliyeadhibiwa kwa kuiingiza
nchi kwenye mikataba mibovu ambayo inapukutisha utajiri wa nchi.
Katika kuonesha kuwa mikataba hiyo ni tatizo, hivi
karibuni Rais Magufuli aliagiza kufanyika mazungumzo ya kurekebisha
mkataba wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Shehena ya Kontena Bandarini
(TICTS), ili uwe na tija kwa Taifa.
Hatua hiyo ya Rais ilikuja miezi mitano baada ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, kubaini Aprili
mwaka huu kwamba kampuni hiyo imevunja mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA).
0 comments:
Post a Comment