Waandishi Wetu
Zitto Kabwe |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali kuhakiki
akaunti na mali za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) na wenzake
waliokuwa katika kamati za fedha za Bunge, ili kubaini kama zinalingana na
kipato walichokuwa wakipata.
Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, amesema
hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, akimuhusisha Kiongozi huyo Mkuu
wa ACT na tuhuma za ufisadi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alipokuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
”Nilikuwa najiuliza hivi chuki ya Zitto kwa Serikali ya
Awamu ya Tano, inayopambana na mafisadi imetoka wapi wakati yeye alikuwa
anasimamia mashirika hayo.
“Miongoni mwa taasisi hizo alizokuwa akisimamia na baadhi
ya marafiki zake ndiyo hao walionunua hekari moja kwa Sh milioni 800, wakati ilikuwa
ikiuzwa kwa Sh milioni 25 na walikuwa wamejificha kwa maslahi binafsi,” alisema
katika ofisi ndogo za Makao Makuu, Lumumba Dar es Salaam.
NSSF ndiyo iliyonunua hekari 20,000 Kigamboni jijini Dar
es Salaam kwa Sh milioni 800 kwa kila hekari, badala ya Sh milioni 25 na
kujikuta katika hatari ya kupoteza Sh bilioni 270, katika mradi wa ujenzi wa
mji wa kisasa wa Dege Eco Village.
Kutokana na tuhuma hizo za NSSF zilizoibuka upya katika
kamati ya PAC wiki hii, Sendeka alisema ni vema Serikali ikague kuona kama akaunti za viongozi wa zamani wa
kamati hizo, maisha yao na mali walizonazo, zinafanana na mapato halali
waliyokuwa wakilipwa.
Alisema alikuwa anaangalia msukumo wa ghafla na mapenzi
ya akina Zitto waliyokuwa wanayapata kwa nchi, kumbe ilikuwa ni kichaka cha
kuficha baadhi ya maswahiba zao wasichukuliwe hatua.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Rais Magufuli
haina nia ya kurudi nyuma katika jambo lolote na kuwa itasonga mbele huku
akiamini kuwa Serikali iliyochaguliwa na watu haiwezi kufa.
“Tunahakika Serikali ya Magufuli iliyopata ridhaa ya
kutumikia watu, haitafutika kwa kelele za mlango wa baadhi ya makuwadi na watu
waliolipwa kuchafua taswira ya Tanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali hiyo itaendelea kushughulikia wakwepa
kodi pamoja na kuchunguza mambo aliyoanzisha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa bandarini.
*Kauli ya Zitto
Akizungumza na waandishi wa gazeti hili, Zitto alisema
hana muda wa kujibu alichoita kuwa ni porojo na viroja vya Sendeka.
Alifafanua kuwa CCM ni chama dola na kuna taasisi nyingi
za uchunguzi za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) na kushangaa kwa nini
vyombo hivyo havisemi, aseme Sendeka?
0 comments:
Post a Comment