Sharifa Marira na Hussein Ndubikile
MILIMA haikutani binadamu hukutana. Ndivyo unavyoweza
kusema baada ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kukutana jana na kupeana mikono katika tukio lililoonekana kukumbusha
mengi kuhusu ‘maswahiba’ hao wa siku nyingi.
Walikutana baada ya miezi 15 tangu Lowassa alipohamia
Chadema baada ya kukatwa CCM katika kinyang’anyiro cha urais na CCM kumpa Rais
John Magufuli dhamana ya kupeperusha bendera yake kwenye mbio za urais.
Lowassa ambaye alijitosa katika mbio hizo, jina lake
lilikatwa na Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Kikwete wakati wa mchakato
wa kura ya maoni kumpata mgombea urais.
Baada ya kutua Chadema na kuuponda mchakato wa CCM kupata
mgombea wake wa urais, Lowassa alipitishwa kwa tiketi ya Chadema na kuungwa
mkono na Ukawa na kwa mara ya kwanza
alizungumzia sakata la zabuni ya kufua umeme ya Richmond, kubainisha kuwa ilitekelezwa kwa agizo kutoka ngazi za juu.
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008
alipojiuzulu kutokana na sakata hilo la Richmond.
Wawili hao ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa
wakirushiana vijembe, walikutana jana katika viwanja vya Karimjee wakati wa
kuaga mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Tukio hilo lilitokea siku 57 tangu waliposhiriki Misa ya
shukrani ya maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya Rais wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Benjamin Mkapa, lakini hakukuwa na
tukio bayana la kukutana na kupeana mikono kama ilivyotokea jana.
Kikwete ndiye alikuwa wa kwanza kufika kwenye viwanja
hivyo saa 3 asubuhi akifuatana na mkewe Mama Salma, na kukaa viti vya mbele kwenye
eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya viongozi.
Wakati Lowassa akiingia kwenye viwanja hivyo sambamba na
mkewe Regina, alisalimu viongozi mbalimbali huku Kikwete akionekana
kuwa makini kumtazama.
Kadri alivyokuwa akisalimia mmoja baada ya mwingine
ndivyo alivyokuwa akikaribia alipoketi Kikwete alisimama na kumpa mkono.
Tukio hilo lilivuta hisia za mamia ya watu waliojitokeza
katika viwanja hivyo pamoja na waandishi wa habari ambao walipigana vikumbo
kupata picha ya wanasiasa hao.
Lowassa ambaye sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alipoulizwa
na JAMBO LEO nini kauli yake baada ya kupeana mkono na Kikwete alihoji: “Sasa
niseme nini?”
Kuzorota kwa uhusiano wa wanasiasa hao wanaoelezwa kuwa
marafiki wa miaka mingi waliopanga mengi pamoja ikiwa ni pamoja na kuwania
urais mwaka 1995, kulitajwa kuibuka kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Licha ya wao au wapambe wao kuzikanusha taarifa hizo,
huku wakati fulani Lowassa akibainisha kuwa hakukutana na Kikwete barabarani,
hali ilikuwa tofauti katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huo hasa baada ya
jina la Lowassa kukatwa.
Kitendo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani kujiunga upinzani
kilifungua ukurasa mpya wa kurushiana maneno, yakianzia kwa Mwanasheria Mkuu wa
Chadema, Tundu Lissu ambaye kwa nyakati tofauti alinukuliwa na vyombo vya
habari akimtaka Kikwete aseme Richmond ni ya nani.
Kauli hiyo ilijibiwa na Kikwete katika kampeni za
uchaguzi huo, akimtaka Lissu kumtaja mwenye Richmond kwa madai kwamba anatembea
naye kwenye kampeni kila siku. Hatua hiyo ilisababisha mwanasiasa huyo naye
kumjibu Kikwete kuwa Richmond ilikuwa yake.
Katika mkutano wa mwisho wa kufunga kampeni, Kikwete
alisema Richmond ilikuwa ya Lowassa na yeye kwa kuwa alikuwa Mkuu wa Nchi
aliruhusu mitambo hiyo kuagizwa lakini akataka sheria ya ununuzi ifuatwe, jambo
ambalo Lowassa na kamati ya makatibu wakuu iliyoteuliwa na Waziri Mkuu,
hawakulizingatia.
Hali hiyo ilionekana kuwa mwanzo wa mwisho wa urafiki wao
wa miaka mingi walioanza pamoja mbio za kuingia Ikulu mwaka 1995 na pia
walipoanza utumishi wa TANU na baadaye CCM, baada ya kuhitimu shahada zao Chuo
Kikuu Dar es Salaam (UDSM) miaka ya 1970.
0 comments:
Post a Comment