Salha Mohamed
Wamachinga Kariakoo |
SERIKALI imepoteza zaidi ya Sh bilioni
100 kutokana na uwepo wa wamachinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa ambao hawalipi
kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hali iliyosababisha kutoa siku 14 waondoke
maeneo hayo.
Hasara hiyo ya Septemba pekee, imetajwa
kutokea baada ya agizo la Rais John Magufuli lililotaka wamachinga wasibughudhiwe.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda alisema jana kuwa hasara hiyo inatokana na wamachinga kushirikiana na
wanaohifadhi bidhaa kwenye maghala na kufunga maduka yao hivyo kutolipa kodi akisema
Ilala peke yake imeingiza hasara ya zaidi ya Sh bilioni 54.
“Sasa wamachinga wameanza kutumika na
waliokuwa na mizigo kwenye maghala na mwishowe tumejikuta mapato yamepungua kwa
TRA mkoani kwetu,” alisema.
Alisema wamachinga hao wamekuwa
wakikiuka sheria na taratibu za kuuza bidhaa nje ya maduka ya wafanyabiashara
wanaostahili kulipa kodi.
Alisema kupungua kwa mapato hayo,
kunatokana na wamachinga hao kuchukua bidhaa na kuingia mtaani kisha kuziuza
kwa bei wanayotaka, huku akibainisha kwamba kwa hali hiyo, uchumi wa nchi
hauwezi kujengeka.
“Nawapa siku 14 wakuu wangu wa wilaya
kuwa mmachinga ambaye hana sehemu ya kufanyia biashara ampe, kwani kila wilaya
imetengewa eneo la wafanyabiashara.
“Nawaomba wamachinga wale ambao wana
maeneo yao warudi kwenye maeneo yao, ambao hawana wawaone wakuu wa wilaya au wakurugenzi
wao watawapangia maeneo husika,” alisema.
Alitoa rai kwa wakuu wa wilaya wake
kuhakikisha kila mmachinga anakwenda sehemu stahiki, kwani zipo za masoko
ambazo ziko wazi lakini hawafanyii biashara kwa kukimbilia barabarani.
Alifafanua, kuwa kwa sasa kila eneo
wamachinga wapo huku wakinyima watu wengine haki ya kutumia barabara hizo, kwa
kupanga bidhaa zao.
Alisema maeneo ya barabarani ni ya
hatari, hivyo wasingependa kuona wamachinga kwenye maeneo hayo na kutoa mwito kwamba
Serikali ilijenga barabara si kwa matumizi ya kupanga viatu na nguo.
“Wafanyabiashara
wenye maduka yao wanashindwa kufanya biashara vizuri kwa sababu mbele ya duka
kuna bidhaa zinazotandikwa chini,” alisema.
Makonda aliongeza kuwa wananchi
wanaofanya ununuzi katika maeneo hayo hulalamika uhalifu sababu mazingira
hayaruhusu kukamata mwizi.
Aliongeza kuwa mbali na kutolipa kodi
lakini wamachinga wamekuwa wakichafua mazingira kwa kuzalisha uchafu na kuuacha
huku wananchi wa kawaida wakishindwa kutembea vema barabarani.
Alisema si vema itumike nguvu kuwaondoa huku
akiwatakia kila la heri katika utafutaji wao wa kipato usio na kero kwa watu
wengine.
“Maeneo ya barabara za mwendo wa haraka
naomba wapishe…Kariakoo yote tulisema barabara ya magari yaendayo haraka
ipitike kirahisi, nako wamevamia hadi barabara ya Ikulu na sehemu zingine za
vituo vya daladala wameviua na kupanga bidhaa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment