Enlesy Mbegalo
Theophil Makunga |
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeiomba Kamati za
Bunge ya Huduma za Jamii kutowasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa
2016 katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 unaotarajiwa kuanza kesho likitaja sababu
tano kutaka ombi lao litekelezwe.
Aidha, TEF limeomba muswada huo uwasilishwe kwenye mkutano
wa sita utakaofanyika Februari mwakani kwa maelezo kwamba linaamini wakati huo
watakuwa wamepata mwafaka wa mambo mengine ya msingi yanayohitaji makubaliano baina
yao.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema jana jijini
Dar es Salaam kuwa wanaomba muda zaidi ili wadau mbalimbali pamoja na
wanahabari wenyewe waweze kujadiliana kwa kina, kwani kuna vifungu na vipengele
vinavyopaswa kufanyiwa marekebisho.
“Kwa hatua ambayo tumefikia hivi sasa, hili
halitawezekana, kwani bado hatujakamilisha mchakato wa majadiliano na utoaji wa
mapendekezo katika ngazi za taasisi zetu,” alisema
Alisema Oktoba 13 mwaka huu, TEF ilipata barua kutoka Ofisi
ya Katibu wa Bunge ikiwaalika kufika mbele ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya
Jamii kwaajili ya kutoa maoni kwenye muswada huo.
Alisema waliitika wito huo na kufika mbele ya kamati hiyo
Oktoba 19, ila kwa kushirikiana na wadau wengine, waliiomba muda wa nyongeza
kwa ajili ya majadiliano zaidi.
Hata hivyo, alisema baada ya muswada huo kusomwa kwa mara
ya kwanza bungeni Septemba 16, walijitahidi kuanza kufanya kazi mapema kadri ilivyozekanavyo.
“Ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa muda, tuliwaarifu
wenzetu katika maeneo mbalimbali nchini kusoma, kuchambua na kutoa maoni na
mapendekezo yao kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” alisema Makunga.
Alisema kazi ya kusoma na kuchambua muswada huo iliyowakilishwa
kwa wataalamu wa sheria, imechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kutokana na
kuwapo na masuala yanayohitaji mjadala mpana kabla ya kufikia hitimisho na
kuyatolea maoni.
Aidha mwaliko wa kamati uliwafikia wakiwa katikati ya
mchakato wa kukusanya maoni, huku timu ya wataalamu ikiendelea kufanya
uchambuzi wa hoja zilizokuwa zimetolewa na wadau wakiwamo wahariri.
Pia, alisema Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari
Tanzania (UTPC), ambao umebeba maslahi ya waandishi wa habari nchi nzima
ulikuwa bado katika hatua ya kukusanya maoni katika ngazi ya mikoa.
“Kwa ujumla sheria inayotugwa ina mambo mengine ambayo
sisi kwa mtazamo wetu hayahitaji uharaka katika kuyafanyia uamuzi, masuala haya
yanahitaji mjadala mpana wa wanataaluma wenyewe na wadau wengine,”
Katibu wa TEF, Nevelle Meena alisema wamesikitishwa na kitendo
cha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba
kusema kuwa Bunge litaendelea na mchakato huo hata kama wadau hawako tayari.
“Tunaomba ieleweke kuwa sio dhamira yetu kukwaza utunzi
wa sheria na wala hatupingi kutugwa kwa sheria hii, ila tunahitaji muda kupitia
muswada h uo kwa makini kuona wapi kuna tatizo gani na liboreshweje, na hii ni
kwa maslahi ya taifa,” alisema
Kamati ya Bunge yakamilisha kazi ya kupitia maoni
Wakati huohuo mwandishi wetu kutoka Dodoma ameripoti kuwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeeleza kuwa imemaliza
kazi yake ya kupitia maoni yaliyowasilishwa na wadau, taasisi na wananchi ili
kuboresha muswada huo.
Mwenyekiti kamati hiyo Peter Serukamba amesema kuwa
wameyapitia maoni yaliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kuna maeneo ambayo
Serikali wameyapokea na kamati inaendelea kuyafanyia kazi.
“Katika miswada ambayo wananchi wameisoma na kusikilizwa
sana ni Muswada huu, maana ndio Muswada pekee ambao kwa kweli umejadiliwa sana
katika vyombo vya habari; kwenye magazeti, kwenye radio na Tv kupitia
vipindi maalum vya kujadili Muswada huu na maoni yao mengi yameingizwa kwenye
Muswada huu,” alisema Serukamba.
Aliyataja maeneo ambayo kamati yake imefanyia kazi na
kuyaingiza kwenye Muswada kama maboresho kulingana na maoni yaliyowasilishwa kuwa
ni pamoja na namna ya kumtambua mwandishi wa habari, namna ya kulinda haki za
waandishi wa habari, kulinda haki za wenye vyombo vya habari pamoja na kumlinda
mtu yeyote katika jamii.
“Mimi na wanakamati wenzangu tunajivunia kwamba
tumeandika historia hii ambayo iliwashinda wengine wote tangu mwaka 1993, sisi
tumeweza kuleta Sheria nzuri ambayo itasaidia waandishi wa habari, itasaidia
tasnia ya habari Tanzania na tutaanza kuwajibika kama taifa na ni mwanzo mpya
kwa uandishi wa habari Tanzania,” alisema Serukamba.
Serukamba amewatoa hofu wadau wa habari juu ya kuanzishwa
kwa sheria hiyo kwa kuwaasa kuusoma muswada huo ambao utaifanya tasnia ya
habari kuwa taaluma.
0 comments:
Post a Comment