Peter Akaro
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harison Mwakyembe |
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, imetoa tamko na mwongozo kuhusu utoaji huduma kwa
makundi maalumu yaliyo hatarini kuambukiza na kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi.
Tamko hilo linakuja baada ya Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk Harison Mwakyembe kueleza kuwapo asasi zisizo za serikali zinazounga
mkono mapenzi ya jinsia moja kwa kusambaza vilainishi, vipeperushi na elimu kwa
siri kwa kivuli cha kutoa afya kwa wanaoishi na VVU.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Waziri wa
Afya, Ummy Mwalimu alisema Wizara yake iliwaita wadau wanaofanya kazi katika
eneo la kupambana na Ukimwi ili kutoa mwongozo kwa asasi zote zinazotoa huduma
kwa makundi maalumu.
“Kwanza ni Serikali kuendea kutoa huduma
bora za kupambana na Ukimwi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, bila kudharau
sheria, mila, taratibu na desturi za Tanzania.
“Pia tutaendelea kutoa huduma bila kubagua
mtu kwa misingi ya dini, kabila, chama au fedha,” alisema.
Waziri alisistiza kuwa suala la kutoa
huduma ya afya kwa makundi maalumu itambulike kwa ujumla si kwa wanaoshiriki
mapenzi ya jinsia moja.
“Pia mdau anayetoa huduma za kupambana
na virusi vya Ukimwi ana wajibu wa kuzingatia sheria za nchi, na kama mdau ni
shirika lisilo la serikali ana wajibu wa kuzingatia sheria za mashirika yasiyo
ya serikali ya kimataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa huduma zinatolewa kwenye
vituo vya afya kwa ajili ya makundi maalumu zitaendelea kwa makundi yote,
isipokuwa wataendelea kuzuia huduma hiyo katika ngazi ya jamii.
“Maana yake shughuli za mashirika yasiyo
ya serikali kwenda kwenye jamii kugawa
vilainishi na kutoa elimu tunazizuia kwa muda hadi utakapotolewa mwongozo,”
alisema.
Alisema Mganga Mkuu wa Serikali
ataongoza kazi ya kupanga wadau katika maeneo watakayofanya kazi nchi nzima.
“Asasi zote zinazotoa huduma ya afya ni
lazima ziidhinishwe na halmashauri husika kabla ya kufanya kazi na asasi zisizo
za kimataifa.
Aliongeza kuwa makundi yaliyo katika
hatari zaidi ya kuambukiza na kuambukizwa Ukimwi ni wasichana na vijana walio
katika umri wa balehe, walio katika mazingira hatarishi, watoto yatima, wanaume
wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
“Pia wapo wanawake wanaofanya ngono
kinyume na maumbile, watumiaji wa dawa za kulevya, wanawake wanaofanya biashara
ya ngono, wafungwa, wakimbizi, wafanyakazi wanaohama kila mara na wafanyakazi
wa migodini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment