Mary Mtuka
Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan |
MRITHI wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu
Rais wa nchi hiyo, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, amesema nchi yake
imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hasa katika
utekelezaji miradi ya maendeleo.
Sheikh Mohamed alitoa ahadi hiyo jana
kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mohamed Al
Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es
Salaam.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo
vya habari Dar es Salaam, ilisema Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana
na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Katika mazungumzo yao, Mkurugenzi Mkuu
wa Mfuko huo, alionesha nia ya kushirikiana zaidi na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu
ya reli na barabara, usafiri wa anga na madini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pamoja na kumshukuru
Mrithi huyo wa Mfalme Rais Magufuli aliialika nchi hiyo kupitia Mfuko wake na
wadau wengine kuja kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo.
Alitaja baadhi ya maeneo ya kuwekeza kuwa
ni ujenzi wa bandari, viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika
ujenzi wa Reli ya Kati ambayo itanufaisha nchi nyingine saba za Afrika
Mashariki na Kati ambazo hazina bandari.
"Tanzania imeamua kujenga Reli ya Kati
kwa kiwango cha kisasa na tayari katika bajeti yetu tumetenga Sh trilioni moja
kwa ajili ya kuanza ujenzi, hivyo tunaukaribisha Mfuko wa Maendeleo wa Abu
Dhabi kushirikiana nasi.
"Wapo wengi waliojitokeza kushirikiana
nasi lakini na nyie tunawakaribisha, mnaweza kuchukua sehemu ya reli na mkajenga,"
alisema Rais Magufuli.
Aidha, Dk Magufuli aliutaka Mfuko huo
kufupisha muda unaotumika kwenye mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili
kuharakisha matokeo yake na manufaa kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment