Mwandishi Wetu
Profesa Benno Ndulu |
HATUA ya Serikali kuhamisha akaunti zake kutoka benki za
biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imetajwa kupunguza zaidi ya Sh
bilioni 673 kwenye benki hizo, huku mabilioni mengine yakitarajiwa kuondolewa.
Taarifa ya Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu kuhusu
mafanikio ya kiuchumi ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, imeeleza
kuwa uamuzi huo mbali na kuondoa fedha hizo, pia umesaidia riba za mikopo
kupungua kutoka wastani wa asilimia 15.49 hadi asilimia 13.87.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo jana, benki nyingi za biashara
zilikuwa zikitumia fedha hizo za umma kununua dhamana za Serikali na hati fungani
na kuifanya Serikali kuuziwa fedha zake, biashara ambayo imeelezwa kuwa sasa imekoma.
Uhamishaji
Uamuzi huo ulitangazwa katika miezi ya mwanzo ya Rais
Magufuli madarakani, ambapo Serikali iliagiza akaunti za mashirika na taasisi zake kwenye
benki za biashara zifungwe na kuhamisha fedha katika akaunti hizo kwenda
akaunti za BoT.
Taasisi za umma zilizohusika na agizo hilo, zilitajwa kuwa
ni pamoja na serikali za mitaa na zingine zote katika mihimili mitatu ya Dola,
yaani Bunge, Mahakama na Serikali Kuu.
Agizo hilo pia lilitaka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za umma, kufunga akaunti zao kwenye benki za biashara na kuhamishia fedha zao BoT.
Agizo hilo pia lilitaka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za umma, kufunga akaunti zao kwenye benki za biashara na kuhamishia fedha zao BoT.
Pia watendaji hao walitakiwa kufungua akaunti ya mapato yao
kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea, kama ni kwa fedha za kigeni au za ndani,
katika tawi la karibu la BoT mara moja.
Baada ya kufungua akaunti hizo, watendaji hao walitakiwa
kuelekeza makusanyo yote ya fedha za ofisi zao, zikiwamo za ruzuku zinazotoka
serikalini kwenda kwenye akaunti mpya zilizofunguliwa kwenye matawi ya BoT,
badala ya akaunti za benki za biashara.
Taarifa ya Serikali yenye agizo hilo, ilisema uhusiano
pekee kati ya mashirika, taasisi na ofisi zingine za Serikali na benki za
biashara, utakuwa ni wa akaunti itakayohifadhi fedha za uendeshaji, ambayo ilitakiwa
kuwa na fedha zinazotosha uendeshaji wa shughuli zao kwa mwezi mmoja tu.
Ukopeshaji
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alikaririwa akisema wakati
mwingine mashirika hayo ya umma hupelekewa fedha nyingi za ruzuku kuliko
mahitaji lya wakati huo na kuziweka katika benki za biashara.
Katika ufafanuzi wake, alisema Serikali ikipungukiwa na
kulazimika kukopa kutoka vyanzo vya
ndani, benki huchukua fedha hizo za ruzuku na kuzikopesha Serikali kupitia
mnada wa hatifungani za Serikali.
“Katika mazingira hayo, Serikali hujikuta ikikopeshwa fedha
zake na wakati wa kulipa mikopo hiyo, hulazimika kulipa na riba ambayo ni fedha
ya wananchi inayotumika kulipa benki hizo, wakati ingeweza kufanya kazi zingine
za maendeleo ya wananchi,” alikaririwa Mafuru.
Fedha zilizoondolewa
Kwa mujibu wa taarifa ya jana ya Gavana Ndulu iliyochapishwa
katika mtandao wa Michuzi Blog, kati ya Novemba mwaka jana hadi Oktoba 26, akaunti
267 zenye amana za Sh bilioni 206.6 zifunguliwa BoT.
“Aidha baadhi ya taasisi hizo zimefungua akaunti za fedha
za kigeni 131, zenye dola za Marekani milioni 163.4, sawa na Sh bilioni 357.69.
Hivyo jumla ya amana zote za shilingi na fedha za kigeni za mashirika na
taasisi za umma zinazotunzwa BoT ni Sh bilioni
564.6,” ilieleza taarifa hiyo.
Mbali na fedha hizo za mashirika na taasisi za umma,
taarifa hiyo ilieleza kuwa pia amana za serikali za mitaa, zimeanza kuhamishiwa
kwenye akaunti maalumu ya BoT kwa ajili ya kutunzwa.
“Mradi huu (kuhamishia amana za serikali za mitaa kwenda
BoT) ulianza kutekelezwa Aprili na mpaka sasa mikoa mitano imeunganishwa.
“Mikoa hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na
Mwanza. Hadi Oktoba 26, amana za halmashauri za mikoa hiyo mitano ambazo ziko BoT,
zinafikia Sh bilioni 108.38. Bila kukamilisha sehemu ya mradi huu, fedha hizi
zingekuwa kwenye benki za biashara,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa haikufafanua kuhusu amana za mikoa
mingine 21, hatua inayoonesha kuwa bado fedha za halmashauri za mikoa hiyo ziko
katika benki za biashara na huenda zitaendelea kuondolewa.
Faida
Akitaja faida za uamuzi huo katika taarifa hiyo, Gavana
Ndulu alisema inasaidia kuweka uwazi kuhusu mapato na matumizi ya mashirika na
taasisi za umma.
Faida nyingine ni kupungua kwa gharama za usimamizi wa
ujazi wa fedha kwenye mzunguko, huku kukiweka usawa katika ushindani wa benki kwani
kabla ya hapo, benki chache ndizo zilinufaika na amana za mashirika ya umma.
Faida nyingine ni benki kulazimika kubuni huduma mpya ili
kujiongeza amana, huku ukuaji wa uchumi ukienda sambamba na ukuaji wa fedha kwenye
mzunguko.
Kutokana na ubunifu wa benki, taarifa hiyo ilisema, riba
za mikopo kwa mwaka zilipungua kutoka wastani wa asilimia 15.49 hadi asilimia
13.87
“Mwenendo huu wa riba ulisababisha kupungua kwa tofauti
kati ya riba za mkopo na za amana kutoka wastani wa asilimia 5.92, ilivyokuwa
miezi tisa ya mwanzo mwaka jana hadi wastani wa asilimia 2.28, miezi tisa ya mwaka
huu, ikimaanisha kupungua kwa gharama za mikopo,” taarifa hiyo ilieleza.
0 comments:
Post a Comment