Suleiman Msuya
SITAKI nataka. Hivyo ndivyo unavyoweza
kusema kuhusu kinachoondelea ndani ya CUF, ambapo upande mmoja ukiweka bayana
kwamba upo tayari kwa mazungumzo ya kumaliza mgogoro, huku upande mwingine
ukieleza hauko tayari.
Kauli hizo zilitolewa kwa nyakati
tofauti jana na pande hizo katika mahojiano na JAMBO LEO, siku chache baada ya
upande unaotajwa kumwunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim
Lipumba na wanachama wengine 11 na kupinga uamuzi wa Msajili kumtambua Lipumba
kama Mwenyekiti wa CUF.
Wakati upande unaomwunga mkono Lipumba
ukieleza kumtambua Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho na kuwa tayari
kwa mazungumzo kumaliza mgogoro ndani ya chama hicho, upande wa Maalim Seif
umeeleza haupo tayari kwa hilo.
Mwenyekiti wa Muda wa Kamati ya Uongozi
CUF, Julius Mtatiro alisema kwa upande wao ni vigumu kufanya mazungumzo na
Lipumba na kundi lake, kwa alichodai si watu wema ndani ya chama hicho.
Mtatiro alisema kwa sasa wanasubiri
taratibu za Mahakama ili kuhakikisha haki inapatikana na kuwa kuzungumza na
Lipumba ni aibu kwa chama na Watanzania ambao wamepoteza imani naye.
Alisema vitendo ambavyo Lipumba na kundi
lake wamefanya vimesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 600 hivyo
unahitajika ujasiri wa hali ya juu kuzungumza mbele ya wana CUF kuwa unahitaji
kukutana nao.
“Mazungumzo na Lipumba ni jambo ambalo
haliwezekani, kwanza tambua kuwa kwa sasa si mwanachama, wala kiongozi kwani
alishafukuzwa na vikao halali, hivyo ili kuzungumza lazima kurejesha hoja yake
kuanzia Kamati ya Utendaji Taifa, Baraza Kuu la Uongozi na Mkutano Mkuu Taifa,”
alisema.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uongozi
alisema kwa tathmini waliyoifanya, Lipumba haungwi mkono na wanachama wengi,
hivyo hana madhara yoyote anayoweza kusababisha ndani ya chama.
Aidha, alisema jambo la kufurahisha ni
kuwa hadi sasa vyombo vya uamuzi ndani ya chama hicho viko upande wa chama
tofauti na ilivyo kwa Lipumba ambaye anaungwa mkono na wachache wasio na uwezo
wa kufanya uamuzi.
Alisema Lipumba anapata huduma kutoka
Serikalini, hivyo ni vigumu kuamini kuwa watakuwa wanafanya mazungumzo na
mwenzao au msaliti.
“Makao makuu ya chama yako salama na
kazi zinaendelea hivyo tunachokifanya sasa ni kuandaa mikakati ya kufanya kazi
katika mikoa ambako mimi nitaongoza operesheni hizo nikiwa na Katibu Mkuu
Maalim Seif na viongozi wengine wacha wao wabaki na ofisi ndogo Buguruni,”
alisema
Mtatiro alisisitiza kuwa katika kuonesha
kuwa Lipumba hana nguvu ni kwenye mchakato wa kufungua akaunti uliokwama hivyo
wanaamini kuwa mwisho wake unafika.
Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi, Abdul Kambaya ambaye yuko kwa Lipumba, alisema wao wako tayari
kuzungumza iwapo nafasi hiyo itapatikana kwani wanachopigania ni CUF na si mtu.
Kambaya alisema katika kuthibitisha
hilo, wamekuwa wakibainisha siku zote kuwa wanamtambua Katibu Mkuu Maalim Seif
na kumtaka arejee ofisi za Buguruni ili wafanye kazi.
“Watu wenye busara ni lazima wasimamie
misingi ya mazungumzo katika kutatua changamoto na migogoro ambayo inawakabili
hivyo wenzetu wakihitaji kufanya hivyo tuko tayari,” alisema.
Mgogoro wa CUF na Lipumba ulianza Agosti
miezi takribani 10 baada ya Lipumba kutangaza kujiuzulu lakini baadaye
akaandika barua ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake.
0 comments:
Post a Comment