Peter Akaro
MABARAZA ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini
yanakabiliwa na upungufu wa watumishi, vitendea kazi na ufinyu wa bajeti na
kusababisha utendaji kuwa mdogo.
Hayo yalibahinishwa jana Dar es Salaam
na Kaimu Msajili wa Baraza hilo, Amina Ntibampemba akisema hiyo ni changamoto
kubwa kwani wanahitaji watumishi 411, kulinganisha na 179 waliopo.
“Tuna upungufu wa wenyeviti, makarani na
wapiga chapa… kuna baadhi ya wilaya wenyeviti wanahudumia mabaraza zaidi ya
matatu au mawili, wengine mkoa mzima,” alisema na kuongeza:
“Hali hii inachelewesha kusikilizwa kwa
mashauri yaliyofunguliwa na wananchi, kutopata nakala za hukumu na mienendo ya
mashauri kwa wakati, hivyo wananchi wengi wanalazimika kufuata huduma mbali za
utatuzi wa migogoro,” alisema.
Amina alisema pia wanakabiliwa na
mazingira yasiyoridhisha kwa kukosa ofisi, maktaba kwa ajili ya rejea za sheria
na ukosefu wa samani na vitendea kazi.
“Hali hiyo inachangia kuchelewa kwa
ukaguzi wa maeneo ya migogoro kutokana na ukosefu wa usafiri,” alisema.
Alisema ili kukabiliana na changamoto
hizo, Serikali inatakiwa kuhakikisha mabaraza ya ardhi yanakuwa na ofisi stahiki,
wenyeviti na kuyapatia vitendea kazi na fedha za kutosha.
0 comments:
Post a Comment