Jemah Makamba
MWANAMUME mkazi wa Ilala, Siwema Seif (40) amehukumiwa na
Mahakama ya Mwanzo ya Ilala kwenda jela mwaka mmoja kwa kumtolea lugha ya
matusi na kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye ni mama yake mzazi.
Akisoma hukumu mahakamani hapo jana, Hakimu wa Mahakama
hiyo, Matrona Luanda alisema ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja ambaye
ni mlalamikaji, ulionesha kukosa shaka na kumtia hatiani mshitakiwa.
Shahidi huyo alisema siku ya tukio mshitakiwa alifika
nyumbani kwao akaomba chakula akajibiwa kuwa kuna wali na mshitakiwa akasema
hataki wali bali anataka ugali na mama akamjibu asingeweza kupika ugali na
kumsisitiza Siwema ale wali.
Zainab alisema baada ya majibizano hayo, mshitakiwa alimtukana
matusi ya nguoni mama yake, huku akisema hawezi kumzaa na kumkashifu, kwamba
hana sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua akiahidi kumtoa roho ndipo amjue
yeye ni nani.
Kwa mujibu wa Zainab, alipoona ugomvi na matusi umezidi aliingia
chumbani mwake, na ndipo mlalamikaji akamfuata na kumtukana huku akitishia
kumwingilia kinyume cha maumbile.
“Baada ya hapo mshitakiwa alinivamia na kunidhalilisha
kimaumbile kwa mikono yake,” alisema.
Baada ya ushahidi wa mama huyo dhidi ya Siwema, Mahakama
ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama ikamtia hatiani.
Karani wa mahakama hiyo, Blanka Shao alisema kwa kuwa mshitakiwa
alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na kitendo alichokifanya ni cha kifedhuli tena
haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake.
Hakimu Luanda alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa
kitendo alichomfanya mama yake mzazi.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda
kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa, nyumba namba 10.
0 comments:
Post a Comment