*Wanufaika wa zamani 93,295 wachekechwa upya
Suleiman Msuya
Mwanafunzi akilia kwa kukosa mkopo |
NUSU ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo ya
elimu ya juu wamekosa, huku mamlaka zikiendelea kuwachunguza wanafunzi wengine
93,295 waliokuwa wakinufaika na mikopo hiyo kuona kama kweli walistahili kupata
au la.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB),
Abdul-Razaq Badru alisema jana jijijini Dar es Salaam kuwa wanafunzi 25,717 wa
mwaka wa kwanza pekee ndiyo watakaopata mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/17 kati
ya wanafunzi 58,000 ambao majina yao yaliwasilishwa kwake na Tume ya Vyuo Vikuu
Nchini (TCU).
Alisema mbali na hilo, bodi hiyo pia inahakiki majina ya
wanafunzi 93, 295 waliokuwa wananufaika na mikopo hiyo ili kujiridhisha kama
kweli walistahili kulingana na vipaumbele vya serikali na watakaobainika kukosa
sifa wataondolewe kwenye mfumo na kutakiwa kurudisha fedha.
Badru alisema kuwa bodi hiyo inatarajia kuhakiki taarifa
za wanafunzi wote wanaondelea na masomo ili kubaini uhitaji wao wa sasa na kwamba
watakaokosa sifa stahili wataondolewa kwenye mfumo wa kukopeshwa.
“Watakaondolewa katika mchakato wa kupata mikopo,
watalazimika kurejesha kiasi walichokopeshwa kuanzia mwezi huu,” alisema Badru.
Alisema katika kutoa mikopo wamekuwa wakitumia vigezo
mbalimbali, vigezo hivyo vitatumika ili wanufaika wanaostahili waweze kupatiwa
mikopo na ambao hawastahili waendelee kujilipia.
Alipoulizwa haoni kama uamuzi huo utaibua mgongano kwa
kuwa wanafunzi hao walianza kupewa mikopo mwaka jana kwa kuzingatia vigezo
ambavyo walikidhi, Badru alisema wanachoangalia kwa sasa ni kujiridhisha na
taarifa ili kuweka mambo sawa.
“Sisi wenyewe watumishi tunahakikiwa, hivyo lengo la
kuwahakiki wanufaika ni kutaka kuhakikisha kuwa wanaostahili wanapata mikopo na
wale ambao wanajiweza wajilipie kama wanasoma masomo yasiyo na vipaumbele,”
alisema.
Badru alisema bodi ya mikopo baada ya kupitia taarifa za
waombaji ilibaini kuwa wapo wanafunzi ambao historia yao inaonesha walisoma
shule za gharama na wanapata mikopo, hivyo ni wakati wa kuachana na kundi hilo
kama litakuwa halina vigezo husika.
Aidha, alisema uhakiki huo utaangalia vipaumbele vya taifa,
familia maskini, yatima, waliosomeshwa na taasisi na walemavu, hivyo wahusika
wakiwa si katika makundi hayo wanaweza kufutiwa mikopo.
Mkurugenzi huyo alisema uhakiki huo unaweza kusaidia wale
ambao walikuwa wanapata mkopo kidogo na wanakidhi vigezo kuongezewa.
Kuhusu wanafunzi watakaonufaika na mikopo alisema bajeti
ya Serikali kwa mwaka 2016/17 ni Sh. Bilioni 483 itahusu wanafunzi 25,717 wa
mwaka wa kwanza na wanaondelea ni 93, 295 ambao watakuwa katika uhakiki.
Alisema hadi sasa wanafunzi wa mwaka kwanza ambao
wamepatiwa mikopo ni 20, 391 na orodha za majina hayo zimetumwa katika vyuo
mbalimbali walivyopangiwa na TCU.
Badru alibainisha mgawanyo wa mikopo hiyo kuwa ni yatima
4,321, walemavu 118, waliofadhiliwa na taasisi 295, wanaosoma kozi za
vipaumbele 6,159 na wanaotoka familia duni 9,498.
Alisema nafasi zilizobakia ni zaidi 4,500 ambazo
zitajazwa na wanafunzi waliokata rufaa na wanaodahiliwa upya na TCU na kuwa
jumla ya wanufaika wapya watakuwa 25,717 kwa mwaka huu wa fedha.
Aidha, alisema idadi ya wanufaika inaweza kuongezeka au
kupungua mwakani hali ambayo itachangiwa na uhitaji na vigezo ambavyo
vitatumika.
Badru alisema ofisi yao itapokea rufaa za waombaji ambao
hawakuridhika na matoke ya upangaji wa awamu ya kwanza na kuwa mchakato huo
utaanza Novemba 2 mwaka huu na kumalizika baada ya siku 90.
Kwa upande mwingine mkurugenzi huyo alitaja waombaji 27,
053 ambao wamekosa mikopo kuwa ni 6,581 hawakuomba mikopo pamoja na kuwa na
sifa, 8,781 waliofuzu kama wahitimu binafsi.
“9, 940 wahitimu waliofuzu kwa vigezo wianishi, 1,416
wasiokamilisha maombi, 245 walimaliza kidato cha tano miaka mitatu iliyopita na
90 wenye miaka zaidi ya 30,” aliongezea
Halikadhalika alisema kuhusu taarifa za wanufaika
walizotuma wakati wa kuomba na kupangiwa mikopo uhakiki utafanyika kwa njia ya
dodoso ambapo kila mnufaika atalazimika kujaza dodoso hilo kwa njia ya mtandao
kupitia akaunti yake.
Kwa upande wake Rais wa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi
wa Fedha (IFM), Kilonzo Mringo alisema bodi ya mikopo inapaswa kutafakari upya
uamuzi wake wa kukutaka kufutia baadhi ya wanafunzi mikopo.
Mringo alisema bodi hiyo inapaswa kuendelea na utaratibu
wa mikopo kwa wanafunzi wanaondelea na kama yapo mabadiliko yahusu wanafunzi
wapya.
Alisema wapo wanafunzi wanalipa ada inayobakia kupitia
fedha za matumizi ambazo wanapewa na bodi hivyo uamuzi huo utagharimu wanafunzi
wengi.
“Mimi nashauri bodi kama inahitaji kuhakiki ihakiki kwa
msingi wa kuangalia au kujiridhisha na wanufaika na si kuwaondolea wanufaika
mikopo hii ni tatizo kwa sababu mikopo hiyo inasaidia sana,” alisema.
Dk. Chris Mauki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
alisema iwapo mwanafunzi analipewa mkopo kulingana na vigezo ambavyo
vilihitajika wakati huo kumuondolea mkopo itakuwa si sahihi.
Alisema kama bodi itabaini kuwa kuna mapungufu au vigezo
baadhi kutofuatwa uamuzi wa kumuondolea mkopo unapaswa kuchukuliwa bi al
kuhurumia mtu.
“Wapo wanafunzi ambao wanadanganya taarifa zao wakati
wakuomba hivyo wakibainika ni sahihi bodi kufanya hivyo ila si sahihi kwa dhana
kuwa hasomi masomo ya kipaumbele je wakati anaomba kulikuwa na mazingira hayo,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment