WAZEE wametajwa kuwa na mtindo wa kuanzisha
uhusiano wa kimapenzi na wasichana wadogo na kuwaambukiza Ukimwi hali inayochangia
vijana hao kuusambaza kwa vijana wenzao na hivyo kuongeza kasi ya
maambukizi.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeeleza dhamira ya
kuwekeza na kutekeleza sera na mipango ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi na
vifo vya uzazi hasa kwa vijana wa kike ambao ndio wamebainika kuwa ni sehemu
kubwa ya wenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Dk. Hamis Kigwangallah alisema hayo mjini Dodoma jana alipozungumza
kwenye semina ya siku mbili ya wabunge kuhusu changamoto za maambukizi ya Ukimwi,
vifo vya uzazi na mimba za utotoni iliyoandaliwa na Mabunge ya Nchi Wanachama
wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi
Tanzania (Tacaids).
Dk. Kigwangallah alisema tahmini iliyofanywa imebainika
kuwa watu wazima wengi ambao tayari wana wenza wao, hupenda kuanzisha uhusiano
na vibinti vidogo ambavyo navyo vina wenza nao na matokeo yake, ugonjwa huo
husambazwa kwa kasi kupitia mzunguko huo.
Alisema tafiti zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa
kuanzia miaka 15 hadi 19 wanaoshiriki kwenye vitendo vya ngono wanazidi
kuongezeka mwaka hadi mwaka, ingawa asilimia 40 ni vijana wa kike na asilimia
47 wa kiume ambao tayari wana ufahamu wa tatizo la Ukimwi.
Alisema Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye kundi la
vijana hasa mabinti wadogo ili kusambaza uelewa, lakini pia kuwaokoa na janga
hilo la Ukimwi.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson,
alisema wabunge wana jukumu la kutumia fursa na wajibu wao wa
kuishauri na kusimamia serikali na kuhakikisha inatekeleza mipango na mikakati
yake iliyojiwekea katika kushughulikia matatizo hayo ya maambukizi ya ukimwi,
vifo vya uzazi na mimba za utotoni.
Alisema wabunge ambao wanashiriki katika vikao vya
bajeti, wahakikishe linapozungumziwa suala la afya ya uzazi, wanawake na vifo vya
akinamama wakati wa kijifungua, mipango yake itekelezwe ipasavyo.
Naye Mkurugenzi wa Miradi na Mshauri wa Sera za Masuala
ya Ukimwi SADC, Boemo Sekgoma aliishauri Serikali iangalie namna ya kutoa
kipaumbele kwa masuala ya afya ya uzazi wa mpango kutokana na ukweli kwamba
takribani asilimia 80 ya bajeti ya masuala hayo inatoka nje ya nchi na wakati
mwingine haitoki kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment