* Apinga kumtambua Lipumba uenyekiti CUF
* AG naye ajumuishwa kwenye kesi hiyo
Grace Gurisha
BODI ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imefungua
kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na kuwasilisha
maombi matatu ikiwamo kutengua barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji
Francis Mutungi iliyotengua uamuzi wa chama hicho wa kutomtambua Profesa Ibrahim
Lipumba kama mwanachama wa chama hicho.
Mbali na Jaji Mutungi na Profesa Lipumba, bodi hiyo imewashtaki
pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju na wanachama wengine 11 wa chama hicho, iliodai walikiuka
taratibu na sheria za chama hicho.
Akizungumza jana nje ya mahakama hiyo baada ya kufungua
kesi, Wakili wa CUF, Hashim Mziray alitaja kesi hiyo kuwa ni namba 23/2016 akieleza
wameifungua kwa hati ya dharura kutokana na mambo yalivyo sasa ndani ya CUF kwani
hawajui hata ofisi zingine zinaendeshwaje.
“Katika maombi hayo tunaiomba mahakama mambo matatu
ambayo ndiyo yanayosababisha kufukuta kwa mgogoro ndani ya CUF tukiomba
yatenguliwe ili shughuli za kisiasa ziendelee,” alisema Mziray.
Alitaja jambo la kwanza kuwa ni kuiomba Mahakama itengue
barua ya Msajili huyo ya Septemba 23 iliyotengua uamuzi wa CUF kumfukuza uanachama
Profesa Lipumba na kumhalalisha kuwa ni mwanachama hai wa chama hicho kama mwenyekiti.
Mziray alisema suala la pili ni kuitaka Mahakama imzuie Jaji
Mutungi kuingilia masuala ya Profesa Lipumba na CUF kwa sababu tayari wao
wameshamfuta uanachama kwa kuwa kazi ya msajili ni kusajili vyama na si
kuingilia mambo ya ndani ya vyama.
“Bodi pia inaomba mahakama hiyo itengue masuala hayo kwa
sababu chama kinataka kufanya siasa, lakini hakiwezi kufanya lolote sasa kwa
sababu kikwazo ni Msajili Jaji Mutungi, tunaomba azuiliwe ili mambo ya CUF
yaendelee,” alisema Mziray.
Akizungumzia sababu za kufungua kesi hiyo kwa hati ya
dharura, Mziray alisema wamefanya hivyo kwa kuwa kinachoendelea ni hatari, hivyo
kutokana na ukweli kwamba hawawezi kufanya jambo lolote wanashindwa kudhibiti ofisi
za chama, ikiwemo ofisi ya Buguruni.
“Wanachama wanashauku kubwa ya kujua nini kinaendelea na
mwafaka ambao umefikiwa ndani ya chama, ndiyo maana tumefungua kwa hati hiyo ya
dharura kwa sababu hivi sasa Mahakama zinasikiliza kesi kwa haraka na kutolewa
uamuzi ndiyo maana wakakimbilia mahakamani,”alisema Mziray
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Hahari wa CUF, Mbaraka
Maragande alisema anashangazwa na Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) kwa kushindwa
kufutilia vitendo vya kijinai alivyodai vilifanywa na vijana wa Profesa
Lipumba.
“Ametekwa kiongozi wa CUF hakuna lolote lililofanyika la
kuwakamata wahusika, lakini cha kushangaza tukio lililokuja nyuma ndiyo
limefanyiwa kazi la kuwakamata vijana wetu 23 na kuwapeleka mahakamani ambao
walikuwa wanatoka Zanzibar kuja kuweka ulinzi huku.
“Leo (jana) tulikwenda ofisini kwa DPP kufuatilia
mashtaka tuliyoyatoa polisi, lakini hatukukuta jambo lolote linalohusiana na
mashtaka yetu. Awali tulikataa kuhojiwa kwa sababu walitaka kutupa kesi
nyingine tofauti, kwa hiyo ZCO na DPP hawatutendei haki katika hili Jeshi la
Polisi linatakiwa lifanye kazi bila kuegemea upande wowote.
Alisema matukio hayo yalifanywa na vijana wa Lipumba
Agosti 21 mwaka huu na Septemba 16 wakiwa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam,
lakini hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa.
Mgogoro ndani ya CUF umeibuka mara baada ya Lipumba
kutangaza kurejea madarakani akifuta barua yake ya kujiuzulu kwenye wadhifa
wake wa uenyekiti wa chama hicho aliyoiwasilisha Agosti mwaka jana.
Mgogoro huo hatimaye ulifika kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa ambaye alitoa mwongozo unaoonyesha kumtambua Lipumba kisheria, huku
upande mwingine unaoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad ukiweka msimamo wa kutomtambua na kumfukuza uanachama.
0 comments:
Post a Comment