Sharifa Marira, Dodoma
MFUKO
wa Pensheni wa PSPF uko kwenye hali mbaya kifedha kutokana na kupata hasara
inayofikia Sh trilioni 11.15 hivyo Serikali imetakiwa kuchukua hatua za haraka
za kuuokoa kwa kulipa madeni yake.
Agizo
hilo lilitolewa juzi na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati inapitia
hesabu za shirika hilo za mwaka 2014/15.
Ripoti
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka huo, zinaonesha
kuwa una hasara ya Sh tilioni 11.15, kutokana na Serikali kuchelewa kulipa
madeni ya mafao ya wanachama waliokuwapo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo
Julai, 1999.
Kwa
mujibu wa taarifa ya CAG shirika hilo lisipookolewa litaelekea kufa kutokana na
ukweli kuwa kwa mwaka huo wa fedha unaoishia Juni 2015, lilipata hasara ya Sh
trilioni 11 badala ya faida.
Wakati
PAC ikipitia hesabu hizo za CAG, ilibaini kuwa pamoja na kupokea michango
ya wanachama wake inayofikia Sh bilioni 661 kwa mwaka, inalazimika kulipa mafao
yanayofikia Sh bilioni 663 na hivyo upungufu wa ulipaji deni hilo kwa Sh
bilioni mbili.
Mbunge
wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema kiasi ambacho Mfuko huo unakusanya na
matumizi yake hasa kwa kulipa mafao hakitoshelezi, kwani kwenye mafao pekee,
kuna upungufu wa Sh bilioni mbili.
‘’Mwaka
2010 walikuwa na nakisi ya Sh trilioni 6.2 na sasa mwaka 2014 imeonekana nakisi
ya Sh trilioni 11.6, hatua za haraka zisipochukuliwa, Mfuko huu unaelekea kufa
wa kuuokoa ni Serikali ambayo inadaiwa,” alisisitiza.
Alisema
mwaka 1999 wakati Mfuko unaanzishwa, Serikali iliupa wafanyakazi takriban 700
ambao haikuwachangia chochote kwenye Mfuko na kukubaliana na PSPF kuwa italipa
Sh bilioni 710.
Alisema
hata hivyo, Serikali haikulipa deni hilo na baadaye iliingia mkataba na Mfuko
kulipa Sh bilioni 71 kila mwaka, jambo ambalo pia halikutekelezwa zaidi ya
kulipwa fedha kidogo na kusababisha deni hilo kukua na kufikia Sh trilioni 2.6.
Mbunge
wa Sikonge, Joseph Kakunda, alisema kwa mujibu wa ripoti ya CAG na deni hilo la
mafao ya wastaafu wa mwaka 1999, pia Mfuko una madai ya mikopo kutoka taasisi
za Serikali ya Sh bilioni 499.7.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dorothy Mwanyika alisema Serikali inalitambua
deni la PSPF, na itaanza kulilipa kupitia njia ya hati fungani kuanzia Februari
mwakani.
Mwanyika
alisema kuhusu deni la wafanyakazi wa mwaka 1999, Serikali itaanza na utaratibu
wa kuhakiki deni hilo ndipo ianze kulilipa kwa kutumia hati fungani za miaka
mitatu hadi 20.
Alisema
malipo hayo yatajumuisha madeni ambayo Mfuko umechangia katika miradi mikubwa
ukiwamo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
0 comments:
Post a Comment