Fidelis Butahe
WAKATI Rais John Magufuli akisuka
serikali yake kwa kuwatumia zaidi vijana, JAMBO LEO limebaini kuwa kundi hilo
limemwangusha, baada ya kulazimika kutengua uteuzi wa wateule 16 katika kipindi
cha miezi minne tu tangu waanze kazi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wamesema
Rais huyo wa Awamu ya Tano anafanya kazi nzuri, lakini alipaswa kuwa makini
katika uteuzi wake ili kupata wasaidizi wataokwenda na kasi yake.
Julai
7 mwaka huu Rais alifanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji
matano, Manispaa 21, Miji 22 na Wilaya 127 za Tanzania Bara. Kati ya
wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 waliteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi
wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya.
Kati yao, wakurugenzi wa Halmashauri za
wilaya 11, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji mmoja na Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa moja walikacha uteuzi huo na hivyo, kumlazimu Rais kuteua wengine
13 kujaza nafasi hizo, mwezi Septemba.
Pia, Septemba 27 mwaka huu, Rais Magufuli
alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda baada ya
kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana
na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo “Kamati Maafa Kagera” kwa lengo la
kujipatia fedha.
Oktoba 18, Rais pia alitengua uteuzi wa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Emmanuel Mkumbo huku Ikulu ikieleza kuwa
atakayeziba nafasi hiyo atatangazwa baadaye.
Uteuzi huo ulitenguliwa ikiwa imepita
siku moja tangu Mkumbo alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro
kwa tuhuma za kutishia kumuua askari wa usalama barabarani mkoani humo, Koplo
Tuti Ndaga.
Tukio hilo lilitokea takribani wiki moja
iliyopita eneo la Mkambarani baada ya mkurugenzi huyo kutakiwa kusimama, baadaye kudai anatumia gari la
Serikali licha ya kubainika kuwa na kasoro kadhaa.
Maoni ya wachambuzi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha,
Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Nadhani ni kwa sababu rais ameleta
watendaji wapya wengi kuziba nafasi za wazoefu…, siamini kama wakurugenzi wa
zamani hawakuwa na sifa nzuri za uchapaji kazi. Siamini kama rais alikuwa na
taarifa zao sahihi.”
“Miongoni mwa watendaji wa zamani, wapo
ambao walipaswa kuachwa huku akiponda uteuzi wa wakurugenzi hao kufanyika
kisiasa, inakuwaje watumishi wa Serikali wanakuwa makada wa chama? Hili
hupunguza uwajibikaji kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Huria (OUT), Hamad Salim alisema: “Kuna sababu mbili, kwanza ni rais mwenyewe
na pili ni watendaji anaowateua.”
Aliongeza: “Katika jambo la kwanza naona
tatizo katika kuchagua majina ya watu ambao rais anapaswa kuwateua. Ukitizama
utaona sura nyingi mpya tofauti na marais waliopita ambao walikuwa na utaratibu
wa kuteua wapya wachache na kuendelea na wale waliowakuta kwa ajili ya
kuendeleza uzoefu.”
Alisema kinachotokea sasa ni ishara kuwa
Rais Magufuli hawaamini watendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne na kutokuwa na
umakini katika kuwachagua wengine kutokana na wengi kuvurunda, kufanya mambo
kinyume na matakwa ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Alibainisha kuwa baadhi ya watendaji nao
wana matatizo kutokana na kushindwa kuenda na kasi ya Rais aliyedai kuwa
anapenda kuona wateule wake watekeleza kile anachokiamini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alipingana na wenzake na kubainisha
kuwa ni jambo jema kwa rais kuwatumbua watendaji wazembe na wanaokiuka
utaratibu wa kazi aliouweka.
“Mwalimu Nyerere (Julius) aliwahi kusema
zamani watendaji walikuwa hawachukuliwi hatua kwa sababu ya uchache wao. Kwa
sasa wapo wengi, hivyo mmoja akiharibu ni vyema akaondolewa na kuwekwa
mwingine,” alisema.
“Rais amekuwa akisisitiza kubana
matumizi na kupambana na rushwa hivyo lazima awe na watendaji wanaokwenda na
kasi ya kupambana na mambo hayo. Ndio maana alimwondoa Kitwanga
(Charles-aliyekuwa Waziri wa Mmabo ya Ndani), kwa ulevi.”
Ends
0 comments:
Post a Comment