Sharifa Marira na Hussein Ndubikile
RAIS John Magufuli ameasa watoto wa marehamu Didas
Masaburi kushikamana.
Alitoa wosia huo jana wakati wa kuaga mwili wa marehemu
Meya huyo wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam kqwenye viwanja vya Karimjee na
baadaye kuzikwa jana Chanika.
Rais Magufuli alisema unapotokea msiba shetani hupata
nafasi ya kujipenyeza kwenye familia na kuwahimiza kuwa wamoja kwa kuwa baba
yao aliwapenda na ndiyo maana hakuwabagua.
‘’Naomba mshikamane, mtoto mkubwa wa marehemu awe
kiongozi wa familia, nafahamu uchungu mlionao msiruhusu shetani aingie ndani ya
familia,” alisema Magufuli.
Awali Rais alisema baadhi ya Waafrika kuwa na wake watano
hadi 10 ni kawaida.
Alitoa kauli hiyo kwa nia iliyoonekana ya kujaribu kuzima
minong’ono na sintofahamu iliyoibuka baada ya wasifu wa marehemu kueleza kuwa
ameacha mke mmoja, wajane na watoto 20.
‘’Tumetambulishwa hapa mke mmoja, lakini mimi nafahamu
wako wanne au watano hivi. Tabia zetu za kiafrika kuwa na wake wanne, watano,
sita au 10 ni kawaida hata Mfalme Suleiman
alikuwa na wake 1,000. Tunamsoma kwenye vitabu (vya dini) hivyo naombeni
mshikamane,” alisema Rais Magufuli.
Baada ya kauli hiyo muda mfupi kabla ya kuanza ratiba ya kuaga mwili, Rais alishangiliwa
kwa kupigiwa makofi na vigelegele na baadhi ya ndugu wa marehemu.
Rais alilazimika kueleza hayo baada ya awali msemaji wa
familia, Machabe Masaburi kwenye wasifu wa marehemu kueleza kuwa ameacha mke wa
ndoa na wajane, bila kutaja idadi yao, jambo lililozua minong’ono miongoni mwa
ndugu na jamaa ambao tangu awali walionekana kukaa kwa makundi.
Rais Magufuli ambaye wakati wasifu wa marehemu ukisomwa
alikuwa akiteta jambo na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alisema: “Najua hata
watoto wako zaidi ya 20…, nilikuwa nateta na Kikwete, tulitamani hata sisi
tungekuwa na wake wa namna hiyo.”
Maelezo ya Machabe yalionekana wazi kuchanganya ndugu huku
baadhi wakisikika wakisema maelezo yake hayakuwa sahihi, lakini hali ilibadilika
baada ya Rais kumaliza kuzungumza.
“Amefanya kitu cha msingi sana kwa kweli, maana hali
haikuwa nzuri hapa,” alisikika akisema mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakuwa
tayari kutajwa jina lake gazetini.
Mwingine aliiambia JAMBO LEO, kuwa Meya huyo wa zamani alikuwa
na wake watano na mmoja aliyejulikana kwa jina la Nyangeta alifariki dunia, na
kubaki wanne ambao ni Janeth, Zulpa, Grace na Anna.
Masaburi ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam
kati ya mwaka 2010 na mwaka jana na kugombea ubunge wa Ubungo mwaka jana alifariki
dunia Jumatano iliyopita.
0 comments:
Post a Comment