Celina Mathew
MSICHANA pekee aliyeingia katika kumi bora ya wanafunzi
waliofanya vizuri kitaifa katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, Justina
Gerald, ameelezea siri ya mafanikio yake.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa simu jana, Justina
aliyesoma shule tatu katika elimu yake ya msingi na kuhitimu katika Shule ya
Msingi Tusiime, alisema moja ya siri ya mafanikio yake ni kujituma katika
kujisomea.
Kwa mujibu wa Justina aliyesoma katika Shule ya Mwalimu
Julius Nyerere kuanzia la kwanza hadi la sita na baadae akahamishiwa Kaizirege,
alikuwa akiamka saa 10 alfajiri kila siku na kujiandaa ambapo huanza kujisomea
saa 12 mpaka saa moja asubuhi.
Baada ya hapo, Justina alisema saa moja huenda kunywa uji
kabla ya kuanza ratiba ya kawaida ya vipindi vya darasani kuanzia saa 2 asubuhi
mpaka saa tisa alasiri, ambapo hutoka kwaajili ya mapumziko ya jioni.
Justina alisema kuanzia saa 10 mpaka 12 hujisomea tena
kabla ya kwenda kula chakula cha jioni, kisha saa moja usiku wanaingia darasani
kwaajili ya vipindi vingine hadi saa mbili usiku.
Kuanzia saa mbili usiku, Justina alisema muda huo amekuwa
akiutumia kujisomea mwenyewe hadi saa tatu
usiku ndipo huingia bwenini kwa ajili ya kulala.
Aliwashukuru waalimu wa Tusiime na kuwashauri wanafunzi
wenzake kuwa na tabia ya kutokata tamaa kwa kuwa ipo siku watafanya vizuri na
kujulikana kitaifa kama yeye kwani fursa zipo hivyo kinachotakiwa ni kusoma
kwa bidii.
Akisimulia alivyopata taarifa ya kufaulu kwake, Justina
alisema alipigiwa simu na baba yake na
kuambiwa kwamba amepigiwa simu na walimu kuwa amefaulu vizuri na kumuahidi kuwa
akirudi nyumbani jioni watazungumza.
Baada ya baba yake kurudi, alisema alimwita na kumpongeza
na kumweleza kuwa atatafutwa na vyombo mbalimbali vya habari ili aelezea siri
ya ufaulu wake hivyo atoe ushirikiano na pia mama yake alimpongeza.
Justina alisema ndoto yake ya baadae ni kuja kuwa
mfanyabiashara maarufu au mhasibu na kilichomvutia ni mama yake na shangazi
zake kufanya shughuli kama hizo.
Mwanafunzi huyo alisema akiwa nyumbani hupendelea kusoma
vitabu vya hadithi kikiwemo cha 'Diary of the Wimpy Kid' na vinginevyo.
Alisema anapenda sana kusaidia watoto yatima na mara
nyingi akiwa nyumbani hupendelea kumsaidia dada yake kuosha vyombo, kudeki,
kufagia, kufua na kazi nyingine za nyumbani.
0 comments:
Post a Comment