Mwandishi Wetu
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa
aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, imebainika
kwamba uchunguzi dhidi ya ujangili uliofanikisha kukamatwa kwa pembe za ndovu
50 ndiyo sababu ya kutumbuliwa kwake.
Habari za ndani kutoka katika vyanzo mbalimbali
zilizolifikia JAMBO LEO zinabainisha kwamba shushushu huyo mkuu alipewa taarifa
za kuwepo kwa pembe hizo, lakini alishindwa kutoa ushirikiano kwa wasaidizi wake.
Inaelezwa kwamba kushindwa kwa bosi huyo kutoa
ushirikiano kuliwasukuma wasaidizi wake hao ‘kumchoma’ kwa kumpa taarifa mkuu
wa nchi (Rais Magufuli).
Inadaiwa kwamba kwa mujibu wa taratibu za utendaji kazi
za kipelelezi, DCI ndiye anayetakiwa kutoa maelekezo katika matukio kama hayo
ya uharamia wa pembe za ndovu, lakini katika tukio hilo Diwani alionesha
udhaifu.
Chanzo chetu cha habari kinadai kuwa baada ya wasaidizi
wake kutoa taarifa za kuwepo kwa mzigo huo haramu naye kutoonyesha ushirikiano
waliwasiliana na wenzao wa Idara ya Usalama wa Taifa, ndipo taarifa zikafika
kwa Rais.
“Baada ya taarifa hizo kufika, Rais alitoa maelekezo kwa
mashushu hao kuendelea na mchakato ili waweze kuwakamata majangili hao, huku
DCI Diwani akiwa hajui nini kinaendelea,” kilieleza chanzo hicho.
Kiliongeza: “Hapa DCI amezungukwa, suala hili tunachojua
aliambiwa lakini akashindwa kuchukua uamuzi. Si unajua biashara hizi ni za
wakubwa, wakati mwingine unabaki kama zuzu, hizi kazi ni ngumu sana ila nyie
mnatulaumu sisi watenda kazi.”
Alisema watu wanaweza kuona kama DCI ni mzembe lakini ni
vyema kutambua kwamba kupambana na biashara hiyo ni lazima kujitoa mhanga kwani
kundi hilo lina nguvu ya kila kitu.
Mtoa taarifa huyo alisema dhana kuwa Diwani ameshindwa
kuendana na kasi ya Rais Magufuli haina uhusiano na tukio la kutumbuliwa kwake
kwani yeye ni moja wa viongozi wa Jeshi la Polisi aliyekuwa akifanya kazi kwa
uadilifu na misingi ya kazi.
Alisema hata suala hilo la pembe za ndovu alikuwa
amejipanga kupata matokeo chanya, ingawa amekumbwa na bahati mbaya.
Diwani ameondolewa katika nafasi hiyo akiwa amefanya kazi
kwa takribani mwaka mmoja na miezi mitano, baada ya kuteuliwa Mei, mwaka jana
na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Alipoteuliwa kushika wadhifa huo aliweka bayana kuwa matarajio
yake ni pamoja na kuona Tanzania inaendelea kuwa na amani na usalama.
Kabla ya uteuzi huo, Diwani alikuwa Kaimu Kamishna wa
Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai na alipoteuliwa kuwa DCI, nafasi hiyo
ilichukuliwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Valentino Mlowola ambaye kwa
sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kabla ya hapo, mwaka 2012, Diwani alihamishiwa mkoani
Mbeya kuchukua nafasi ya Kamanda Advocate Nyombi na kuwa kamanda wa polisi wa
mkoa huo.
Kabla hajawa RPC, aliwahi kushika nafasi nyingine za
kiutendaji na kiutawala kama mlinzi wa IGP mstaafu Omari Mahita, Kaimu Mkuu wa
Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga.
Juzi kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi
alitoa taarifa ya kutengua uteuzi wa Athuman huku kukiwa hakuna sababu ya
utenguaji huo iliyoanishwa.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa DCI Athuman atapangiwa
kazi nyingine na kuwa uteuzi wa DCI mwingine atatangazwa baadaye.
0 comments:
Post a Comment