Hussein Ndubikile
WANAFUNZI 1,780 wa mwaka wa kwanza wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),
wamepewa mikopo na Serikali.
Hatua hiyo imekuja baada Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa juzi kutangaza kuwa hadi leo asilimia 90 ya wanafunzi wa elimu
ya juu wanaostahili mikopo watakuwa wamepata.
Kwa mujibu wa Serikali UDSM ina
wanafunzi 3,666 wa mwaka wa kwanza wanaostahili mikopo, huku IFM ikiwa na
wanafunzi 2,000.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati
tofauti viongozi wa Serikali za wanafunzi wa vyuo hivyo walisema Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) juzi ilianza kupeleka majina ya wanafunzi
wanaopata mikopo huku wakisitiza kuwa kitakachofuata ni mchakato wa kusainisha
wanafunzi hao.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa
UDSM (Daruso), Boniphace Emmanuel alisema Ijumaa iliyopita Bodi hiyo ilipeleka
majina 646 ya wanafunzi huku jana yakipelekwa mengine 900 na kufanya idadi kuwa
1,546.
Alisema wanafunzi wapatao 11,000
wanaoendelea na masomo ya shahada mbalimbali bado majina yao hayajawasilishwa
chuoni hapo na walipojaribu kufuatilia, waliambiwa suala lao linashughulikiwa
na Bodi.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IFM
(IFM-SO), Kilonzo Mringo alisema kabla Waziri Mkuu hajatoa tamko lake, Bodi ya
Mikopo ilishapeleka majina 240 huku akiongeza kuwa walishauri wanafunzi
wasisaini mpaka watapojua hatima ya majina ambayo hayajapelekwa.
Alisisitiza kuwa wanafunzi 2,864 wa
mwaka wa pili na wa tatu majina yao hayajapelekwa hali inayofanya
waliofika kuanza muhula kuishi kwa tabu huku wanaotoka mikoani wakisita kuripoti
kukwepa ukata huo.
0 comments:
Post a Comment