MOI yaomba kuchangiwa damu



Salha Mohamed

TAASISI ya Tiba ya Mishipa ya Fahamu (MOI), imewataka wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.

Taasisi hiyo iliyokatika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), yenye watoto 40 waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji,ikiwa ni maadhimisho katika kuelekea kilele cha siku ya watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa duniani, Octoba 25 kila mwaka.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma katika taasisi hiyo, Jumaa Almasi alisema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 4000 huzaliwa wakiwa na matatizo hayo kila mwaka.

 “Maadhimisho hayo yataadhimishwa kwa kuchangia damu Octoba 24, kama mnavyofahamu kuwa upasuaji unahitaji damu, hivyo kwa kushirikiana na Chama cha Wazazi wenye watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa (Asbhat), kuchangia damu,”alisema.

Alisema  kwa sasa idadi ya watoto wanaofika hospitalini hapo  na kuonana na madaktari imeongezeka kutokana na elimu wanayopata wazazi.

Alisema kumekuwa na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto wao hospitali huku watoto wa mikoani wakipatiwa matibabu kutokana na Kambi ambazo zipo kila mkoa.

“Wananchi wajitokeze kutoa damu ili tufanikishe zaidi ingawa sisi mara kwa mara huwa tunafanya upasuaji hapa na kambi zilizopo mikoani pia lakini wanaohitaji uangalizi huletwa hapa,”alisema.

Almasi alisema mkoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi na Mtwara imeonekana kuwa na wagonjwa wengi kutokana na muamko wa wazazi kupeleka watoto wao hospitali.

Aliwataka wanawake wanaotarajia kubeba mimba kujiandaa kabla ya kubeba ili kuepuka matatizo ya kujifungua motto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.

“Wajawazito wafuate masharti wanayopewa na madaktari kufuata ulaji mzuri wa kula vyakula vya ziada na madini ya Folic Acid,”alisema.

Almasi alisema wapo wazazi wasiowarudisha watoto wao kuangaliwa pindi wanapopata matibabu ya awali kwa kukosa fedha za kusafiri hasa wa mikoani.

“Utakuta wagonjwa wengine tunaopata wamefika hapa kutokana na kupata michango kutoka misikitini au makanisani na wakipata matibabu.

“Na wakipangiwa siku ya kurudi kuangaliwa hawarudi tena hivyo  tunakuwa hatujui maendeleo ya watoto wao,”alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo