Dalila Sharif
Isack Ernest |
NI kama mauzauza ya kijana, Isack Ernest,
aliyepigwa akishukiwa kuwa mwizi kiasi cha kudhaniwa amekufa na kupelekwa mochari
ya Hospitali ya Temeke.
Wakati kijana huyo akisimulia mkasa
uliomkuta mwanzoni mwa wiki iliyopita, jana baba yake aliieleza JAMBO LEO alivyopata
taarifa hizo zilizozua taharuki katika familia yake.
Hata hivyo, wakati baba huyo, Ernest
Chalo akieleza mkasa mzima ikiwa ni pamoja na msimamizi wa mochari kumvua nguo
maiti mwingine na kumvisha Isack anayedaiwa kuzinduka chumbani humo, Mganga
Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Agustino Mosha alisema katika hospitali hiyo
hapakuwa na maiti aliyezinduka mochari.
Kwa upande mwingine Jeshi la Polisi nalo
likigoma kueleza Isack alivyokuwa alipopokewa, kwa madai kuwa ni kazi ya
madaktari.
Jumamosi iliyopita, kijana huyo wa
kidato cha tatu wa sekondari ya Lumo
alipigwa na wananchi akidaiwa kuhusika na tukio la uporaji wakati akirejea
nyumbani baada ya kuangalia tamasha la muziki wa Singeli, Mbagala Zakheim.
Katika tukio hilo, kijana Seleman Hamisi aliuawa.
Dk Mosha alisema siku ya tukio walipokea
maiti wawili, Selemani Selenge (16) ambaye mwili wake utasafirishwa kwenda Musoma
na Kelvin Ally (14) ambaye mwili wake ulichukuliwa Oktoba 17.
Alibainisha kuwa hakuna kijana
aliyefikishwa mochari na kuzinduka.
“Katika hospitali kuna utaratibu wa kupima
maiti; mapigo ya moyo na mboni za macho ili kujua kama mtu amekufa au la. Ni
kinyume cha sheria kuhifadhi mochari mtu hai,” alisema.
"Navisihi vyombo vya habari visitoe
taarifa za uongo kwa jamii wakati havijazifanyia kazi kujua ukweli wake,”
alisema daktari huyo katika mahojiano.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Temeke,
Gilles Murato alipoulizwa kuhusu habari hizo, alisema hawezi kuzungumzia
masuala ya hospitali.
Baba
Akizungumzia tukio hilo, Chalo alisema
akiwa nyumbani alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akimtaka aende hospitali ya
Temeke na nguo za kumvisha mwanawe ambaye alizinduka akiwa mochari baada ya
kufikishwa hapo na Polisi.
“Baada ya taarifa hiyo nilishituka kwa
kweli. Nilimtafuta Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na baada ya kufika hatukuona
mwili zaidi ya kushuhudia gari la Polisi likiondoka,” alisema.
"Nilipokwenda mochari, nilikuta mtu
mmoja na kunieleza kuwa yeye ndiye msimamizi wa chumba hicho na kwamba mwanangu
alizinduka hivyo yeye akamvua nguo maiti mwingine ili kumsitiri (Isack).”
0 comments:
Post a Comment