Enlesy Mbegalo
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli ametaka mawaziri wa Mambo
ya Nje wa Kenya na Tanzania kukutana kabla ya mwisho wa mwaka huu kujadili
usalama wa nchi hizo, huku akitaka wafanyabiashara wa Kenya kuja kuwekeza nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mwasiliano ya Rais
Ikulu kutoka Kenya, Rais Magufuli alisema kutokana na ujirani uliopo kati ya
nchi hizo, ni lazima usalama uimarishwe.
“Ni lazima mawaziri wa Kenya na Tanzania wakutane kabla
ya mwaka huu kwisha ili wajadili mambo ya usalama wa nchi hizi,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema ziara hiyo inampa fursa ya kujenga upya uhusiano wa
Tanzania na Kenya katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuimarisha biashara kati ya
mataifa hayo mawili.
“Hii ni kuthibitisha kuwa Watanzania na Wakenya ni ndugu mfano
Kenya kuna Wamasai na Tanzania wapo pia lakini wanapotaka kulisha mifugo yao
lazima waangalie mipaka,” alisema Dk Magufuli
Aliwataka Wakenya kuwekeza biashara zao Tanzania kwa
lengo la kukuza uchumi wa nchi hizo.
“Nchi ya kwanza ya kiafrika yenye uwekezaji mkubwa Tanzania
ni Kenya, hakuna nchi nyingine ya kiafrika zaidi ya hii,” alisema.
Alisema Kenya ni nchi rafiki namba moja katika Afrika
ambayo imewekeza zaidi ya kampuni 526 kwa wastani wa dola za bilioni 1.7 za
Marekani.
“Kampuni hizo zimeajiri Watanzania 59,260. Takwimu hizi
zinaifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza ya kiafrika yenye uwekezaji mkubwa
nchini,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa jumla ya thamani ya biashara kati ya Tanzania
na Kenya imeongezeka kutoka Sh bilioni 600 mwaka 2010 hadi Sh trilioni 2. 044
mwanzoni mwa mwaka huu.
Rais Uhuru Kenyatta alitaja suala ya mawasiliano kuwa ni
moja ya watakayoshirikiana na kwamba mawaziri wa mambo ya nje wa Kenya na
Tanzania watakutana kupanga mambo ya majeshi, kuimarisha usalama.
0 comments:
Post a Comment