Hussein Ndubikile
NI balaa. Ndivyo unavyoweza kusema baada
ya maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kushindwa kujisajili kutokana na
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuchelewesha mikopo hadi jana, siku tatu
tangu vyuo hivyo vifunguliwe.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
katika vyuo kadhaa Dar es Salaam, umebaini kuwa baadhi ya wanafunzi hao
wanaranda mitaani wakisubiri mkopo huo ambao kuchelewa kwake kumefanya hata
vyuo vishindwe kuwahudumia.
JAMBO LEO ilishuhudia wanafunzi hao
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tumaini, DUCE, Ardhi na Muhimbili
wakisotea usajili chuoni hapo, huku wengi wakieleza kukwama kwa siku ya nne
jana.
UDSM na Tumaini vilifunguliwa Oktoba 10,
lakini baadhi ya wanafunzi wanaotoka mikoani walilazimika kufika Dar es Salaam
tangu Oktoba 8 kuwahi usajili.
Hata hivyo, walipofika chuoni, wengi
walishindwa kujisajili baada ya kuelezwa kuwa Bodi ya Mikopo haijawaingizia
fedha, hivyo kulazimika kuzunguka mitaani wakisubiri fedha hiyo.
Mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Elimu
kutoka Iringa, Primus Kola alisema
aliwasili Dar es Salaam Oktoba 8 kuwahi usajili UDSM. Alisema tangu
afike hajaambiwa ni lini majina ya kugawiwa mikopo yanafika.
Mwanafunzi huyo aliyeeleza kuwa yuko
katika hali ngumu kifedha, alisema: "Nilifika tangu Oktoba 8 hadi sasa
sijajua hatima yangu ya mikopo na hapa sina ndugu wa kwenda kuishi kwao."
Mwanafunzi mwingine wa Shahada ya
Sheria, Said Ally alisema haelewi kwa nini Bodi haijaleta majina ya wanafunzi
wanaotakiwa kupewa mikopo na hana fedha za kumwezesha kufanya usaili.
"Huwezi kupata sehemu ya kulala
bila kulipia fedha hata usajili wa kozi yako inakuwa vigumu," alisema.
Mwanafunzi mwingine wa mwaka wa kwanza Shahada
hiyo kutoka Mwanza, Halima Sudi alisema bado hajajua siku ambayo majina
yatawasilishwa chuoni na hilo linaendelea kumpa wakati mgumu.
Waziri wa Mikopo wa Serikali ya
Wanafunzi wa UDSM (DARUSO), Eliud Kasunzu alisema aliambiwa kilichochelewesha
majina hayo ni kutokana na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuchelewesha mchakato wa
ushughulikiaji wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo.
Alisema baada ya kufuatilia Bodi ya Mikopo
waliambiwa ndani ya wiki hii au wiki ijayo majina hayo yatawasilishwa chuoni hapo.
Alifafanua kuwa endapo Bodi hiyo haitapeleka majina hayo watakwenda wizarani
kujua hatima ya wanafunzi hao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari Elimu na
Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo, Cosmas Mwaisobwa alisema anafahamu vyuo vimeanza
udahili bila orodha ya majina ya wanaostahili kupata mikopo.
"Ninachoweza kusema ni kwamba
tunafahamu tatizo hilo na Bodi inaendelea na mchakato wa kukamilisha majina na
kuyawasilisha vyuoni," alisema.
Alipoulizwa anadhani lini majina hayo
yatakuwa tayari, alijibu: “Siwezi kusema lini kazi hii itakwisha ila muhimu ni
kujua kuwa tatizo linajulikana na Bodi iko katika hatua za mwisho kukamilisha
orodha ya majina."
0 comments:
Post a Comment