Fidelis Butahe
UTANI uliotolewa juzi na Rais John
Magufuli kuhusu idadi tofauti ya wake wa aliyekuwa Meya wa Jiji Dar es Salaam,
marehemu Didas Masaburi umeibua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii.
Watu wa kada mbalimbali walitoa maoni
yao katika mitandao ya Twitter, facebook na Instagram waliungana na mkuu huyo
wa nchi kwa maelezo kuwa utani huo huenda ukamaliza mpasuko wa familia ya
marehemu, wengine wakitofautiana naye kwa madai kuwa utaleta vurugu zaidi.
Kauli hiyo ya Rais iliibua vicheko,
minong’ono na mjadala miongoni mwa mamia ya waombolezaji waliojitokeza kuaga
mwili wa Masaburi aliyefariki Jumatano iliyopita, wale waliokuwa na nyuso za huzuni,
ghafla walianza kutabasamu na kumpigia makofi.
Rais huyo wa Awamu ya Tano alitoa kauli
hiyo baada ya mdogo wa marehemu, Joackim Machabe kusoma wasifu ambao pamoja na
mambo mengine, alisema kaka yake alifunga ndoa na Janeth Masaburi, lakini
ameacha wajane, watoto 20 na wajukuu kadhaa.
Katika ufafanuzi wake, Rais alisema
marehemu alikuwa na wake wanne au watano na watoto zaidi ya 20, huku akiwataka
watoto hao kushikamana huku akitumia Biblia Takatifu kutoa mfano wa mfalme
Suleiman aliyekuwa na wake na watoto wengi.
Katika mtandao wa facebook, Rehema Msami
alisema, “baada ya kusikia mtu akitumia maandiko ya Suleiman kuwa na wake wengi
ili kuhalalisha uovu…, nilitamanai mtu huyo angetumia maandiko ya Suleiman
alipoomba hekima kutoka kwa Mungu,” alisema.
Katika moja ya mijadala iliyoibuliwa katika
mtandao wa facebook kuhusu suala hilo, Ruth Kowero aliandika, “kufa ni kufa na
kila mtu atakufa na ukweli utabaki pale pale, alichokifanya Rais ni nafuu kwa
familia.”
0 comments:
Post a Comment