Salha Mohamed
Shekhe Abubakar Zubeir |
MUFTI Mkuu wa Tanzania, Shekhe Abubakar
Zubeir, amesema huenda muda wa Tume aliyounda kuchunguza mali za Waislamu nchini
ukaongezwa.
Tume hiyo iliyoundwa Agosti 10 yenye
wajumbe wanane ilitokana na agizo la Rais John Magufuli Julai 6 kwenye Baraza
la Iddi akitaka kuunda timu ya kufuatilia kadhia ya mali za Waislamu zilizo
chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Akizungumza jana na JAMBO LEO, Shekhe Zubeir
alisema bado Tume haijamaliza uchunguzi na ikimaliza wautaweka wazi.
“Bado Tume inaendelea, bado muda na
ukiangalia kazi ya kuchunguza si ndogo ni kubwa na huenda tukawaongeza muda wa
kazi hiyo,” alisema.
Alisema kulingana na kazi inayofanya Tume
hiyo, si ya siku mbili au tatu, hivyo inahitaji muda hasa
ikizingatiwa kuwa inazunguka nchi nzima.
Alisema mbali na Tume hiyo kufuatilia
nchi nzima kwa kutembelea sehemu husika, hivyo jamii inapaswa kuiombea imalize kwa
mafanikio.
Mwezi jana, Makamu Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Shekhe Issa Issa aliwataka wananchi wenye taarifa za mali za Waislamu
zilizo chini ya usimamizi na umiliki wa Bakwata, kuwasilisha kwenye Tume.
"Mwenye taarifa zozote za nyaraka
au wenye taarifa za ushahidi wowote wa ubadhirifu wa mali za Waislamu zilizo
chini ya usimamizi na umiliki wa Bakwata awasilianena Tume ya Mufti," alisema.
Alisema katika kufanikisha jukumu hilo,
Tume inafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu na vyombo mbalimbali kufanikisha jukumu hilo huku
akiahidi na kuhakikishia Waislamu na Watanzania kuwa Tume hiyo ni huru inafanya
kazi zake bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote.
Alisema itafuatilia misamaha ya kodi zilizoombwa
na Baraza na taasisi zake nchi nzima, mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na
mali za Baraza na taasisi zake nchi nzima, kuona uhalali wa umiliki huo.
Pia alisema itafuatilia mikataba yote
ambayo Baraza na taasisi zake zilizoingia na wawekezaji na kuona mikataba hiyo
kama ina maslahi kwa Baraza na taasisi zake, lakini pia kuona hali ya usajili
wa mali hizo.
"Pia Tume itafuatilia mapato na
matumizi ya Baraza na taasisi zake na kupeleka taarifa na mapendekezo hayo kwa
Mufti ndani ya siku 90," alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kumaliza
kukusanya taarifa hizo wataziwasilisha kwa Mufti na ofisi yake itaweka hadharani taarifa hiyo ikiwa ni pamoja na
kuchukuliwa hatua stahiki.
0 comments:
Post a Comment