Joyce Kasiki, Dodoma
SERIKALI
inashindwa kuyafutia hatimiliki mashambapori mengi ambayo hayajaendelezwa baada
ya kubaini kuwa yamekopewa mabilioni ya fedha kutoka taasisi za kibenki hapa
nchini.
Hata hivyo, imezihadharisha
taasisi za kibenki kuwa makini kwani endapo zitatoa mikopo kwa dhamana ya mashamba
na yakaleta migogoro kwa kutoendelezwa, itazishughulikia.
Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliitoa kauli hiyo mjini
hapa jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Utalii, wakati akijibu hoja za wabunge baada ya Serikali kuwasilisha
taarifa ya ardhi kuhusu hatima ya matumizi ya mashamba makubwa
yaliyotelekezwa.
Hata hivyo,
alisema ni jukumu la Serikali kulinda umiliki halali kwa watu wenye hatimiliki badala
ya kuwanyang’anya mashamba kiholela.
“Rais ametupa jukumu
la kuhakikisha tunafuta mashamba yasiyoendelezwa, na kazi hiyo inaendelea,
lakini tunafuata sheria ili tusijeshitakiwa," alisema Lukuvi.
Alisema wakati
wakiendelea na utaratibu wa kufuta mashamba yasiyoendelezwa, walibaini kuwapo
mengi yenye mikopo kutoka taasisi za kibenki na hivyo lazima wafuate taratibu
ili benki zisifilisiwe.
Waziri huyo
alisema katika mashamba hayo kuna yaliyochukuliwa mikopo nje na ndani ya nchi
na orodha yote wanayo na wanaendelea kuifanyia kazi kikamilifu.
Alisema wakati
taasisi za kibenki zikijigamba kushiriki katika sekta ya kilimo, zimekuwa
zikishindwa kuangalia uhalisia ikiwa ni pamoja na kufika kwenye mashamba husika
kuona kama yanaendelezwa.
"Mkakati wa
wizara yangu hivi sasa, ni kukutana na taasisi za kibenki zote ambazo mashamba
hayo yamekopea, ili tuweze kufanya mazungumzo na kuona namna bora ya
kumaliza mgogoro huo,” alisema.
Alitolea mfano wa
shamba lililokopewa dola milioni 16 za Marekani mara nane, na hivyo kusababisha
ugumu wa kazi hiyo.
Lukuvi alisema kwa
bahati mbaya licha ya mikopo hiyo kukopwa kwa dhamana ya mashamba lakini
haitumiki kuwekeza kwenye mashamba bali kwenye biashara nyingine ikiwamo
kujenga nyumba za kupangisha nje ya nchi.
Alisema, endapo
ingekuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, sekta ya kilimo nchini
ingekuwa na mafanikio makubwa.
0 comments:
Post a Comment