Joyce Kasiki, Dodoma
Deo Nsokolo |
WADAU wa habari
nchini, wameiomba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii
kuwaongeza muda hadi Februari mwakani.
Lengo ni ili wajadili
kwa kina Muswada wa Huduma za Habari wa Mwaka 2016 kwa manufaa ya waandishi wa
habari na Taifa kwa jumla.
Wakizungumza na
waandishi wa habari baada ya kukutana na kamati hiyo na kutoa hoja hiyo jana,
wadau hao walisema muda waliopewa kuujadili ni mfupi, hivyo kuhitaji muda wa
nyongeza ili kuwafikia wadau wengi hasa wanahabari ambao ndio walengwa wa
sheria tarajiwa.
Rais wa Muungano
wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo alisema
wadau wa sekta ya habari ni wengi hivyo si rahisi kuwafikia wote kwa muda
uliowekwa na kujadiliwa kwenye Bunge lijalo.
"Muswada
huu una wadau wengi, lakini wadau wakubwa ni wanahabari wenyewe ambao
wanahitaji muda wa kutosha kuujadili na kutoa maoni yao, bila hivyo utawaathiri
wao na jamii kwa jumla.
“Tunamwomba
Waziri husika aliangalie wazo hilo, lakini kimsingi hatupingi kutungwa sheria
hiyo kwani ina manufaa kwa wanahabari pamoja na kulinda taaluma ya habari
nchini," alisema Nsokolo.
Rais wa Chama
cha Wanasheria Tanzania (TLS), John Seke alisema chama hicho kimeona bado wadau
wa habari wanahitaji nafasi ya kujadili
Muswada huo ili upate maoni ya kutosha.
Meneja Programu
kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike alisema licha ya kuwa
sheria hiyo iliombwa na wadau hao kutokana na sheria zilizopo kuwa kandamizi, wanahitaji
muda zaidi wa kuujadili.
"Kwa muda
mrefu tasnia ya habari tumekuwa kwenye mchakato, sheria hii tuliiomba, tulisema
zilizopo ni kandamizi kwa hiyo tukasema tushirikiane na Serikali
tuwe na sheria zitakazosaidia kukuza tasnia ya habari, uhuru na uwezo wa
vyombo vya habari kuchangia mchakato wa kukuza demokrasia nchini,
"Na bahati
nzuri tangu mwaka 2006 wadau tulitoa maoni na mwaka 2011 tukaboresha maoni na
leo tumepata Muswada, una mambo mengi ambayo yataathiri waandishi wa habari, wanamiliki
wa vyombo vya habari na wanaotusaidia kwenye kazi zetu za habari, tunapenda
kupata muda ili tufikie maelewano na kupata hiyo sheria," alisema
Mtambalike.
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari, Henry Mahanika alisema kuomba muda wa nyongeza si kuuchelewesha wala kuupinga.
"Si mbinu
ya kuchelewesha au kupinga sheria hii isiwepo na ndiyo sababu tukaomba tupate
muda kidogo tu kwa sheria hii ambayo imeanza mchakato kwa takribani miaka 10.
“Miezi minne
tuliyoomba si muda mrefu na hiyo ni kutaka kujiridhisha ili wadau wapitie na
kuona kama kuna vipengele ambavyo haviendani na sera wala Katiba na waweze
kutoa maoni yao," alisema Mahanika.
Makamu
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema wadau walianza
kukutana Septemba hadi Oktoba na wanaona kila sababu ya kukusanya maoni ya
wadau hususan wanahabari wa mikoa yote nchini.
Alisema
lengo la ushirikishwaji huo na kuomba muda huo hadi Februari ni kutengeneza
sheria ambayo haitapitwa na wakati, haitaonea mtu na wakati mwingine kuipeleka
tasnia mbele zaidi kadri teknolojia inavyokua.
Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Peter Serukamba aliendelea na kikao na kusoma maudhui ya sheria
hiyo pamoja na mchakato wake katika hatua zote na baada ya kumaliza kusoma
akataka wadau waanze kutoa maoni yao.
0 comments:
Post a Comment