Grace Gurisha
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imempandisha
kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA), Ephraim Mgawe na vigogo wengine watatu wa Mamlaka hiyo wakidaiwa kuomba
rushwa ya dola milioni nne za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni nane.
Vigogo hao wanadaiwa kudai na kupokea rushwa hiyo ili
watoe zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta.
Mbali na Mgawe, vigogo wengine ni Mkurugenzi wa zamani wa
Uhandisi TPA, Bakari Kilo (59), aliyekuwa Meneja wa Mazingira TPA, Theophil
Kimaro (54) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya
(60).
Vigogo hao walipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,
ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiana na Wakili
wa Takukuru, Emmanuel Jacob walidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka mawili ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Jacob alidai kuwa mashitaka ya kuomba rushwa yanawakabili
Mgawe, Kilo na Kimaro, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti
na maeneo tofauti ambayo hayafahamiki kati ya mwaka 2009 na 2012.
Ilidaiwa kuwa kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ya
dola milioni nne kupitia wakala wa kampuni ya DB Shapriya ili kuiwezesha kampuni
hiyo kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji
Mwema ya TPA kinyume na sheria ya Takukuru.
Alidai walifanya hivyo ili Shapriya ashinde zabuni
iliyokuwa ikishindaniwa namba AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba
hilo kwenye rasi ya Mjimwema.
Katika mashitaka ya pili dhidi ya Shapriya peke yake,
ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009 akiwa Mkurugenzi wa
DB Shapriya, alitoa rushwa ya dola milioni nne kwa vigogo hao, ikiwa ni kishawishi
kuiwezesha kampuni ya Leighton Offshore Pte kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la
kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji Mwema.
Inadaiwa mtuhumiwa alitoa kiasi hicho cha dola kwa Mgawe,
Kilo na Kimaro ili kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni hiyo.
Baada ya kusomewa mashitaka, walikana kuhusika. Wakili
Jacob alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa
na pia kuwa hawana pingamizi dhidi ya dhamana.
Vigogo hao walinusurika kwenda rumande baada ya kutimiza
masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu waliosaini bondi ya
Sh milioni 500 kila mmoja kiasi hicho hicho.
Hata hivyo, Mgawe si mara yake ya kwanza kupandishwa
kizimbani katika Mahakama hiyo, kwani tayari ana kesi ya matumizi mabaya ya
madaraka akishitakiwa pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Hamad Koshuma.
Ilidaiwa kuwa Desemba 5 mwaka 2011, washitakiwa wakiwa
watumishi wa PTA, katika utendaji wao wa kazi kwa makusudi walitumia madaraka
yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.
Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, ikiwa kwenye hatua ya mwisho ya kutolewa hukumu.
0 comments:
Post a Comment