Fidelis Butahe
Boniface Jacob |
SIKU tano baada ya kuahirishwa kwa
uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mkurugenzi wa Manispaa
hiyo, John Kayombo ameitisha tena uchaguzi huo Jumanne ijayo.
Uchaguzi huo uliahirishwa baada ya
kususiwa na vyama vinavyounda Ukawa kwa madai ya kupewa taarifa ndani ya muda
mfupi, kuongezwa kinyemela kwa idadi ya madiwani na kupinga ‘uhuni’ uliofanyika
katika uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni, baada ya wateule wa Rais nao
kuruhusiwa kupiga kura.
Kwa mujibu wa barua ya Kayombo ya Oktoba
24 kwa madiwani wote wa Manispaa ya Ubungo, kutakuwa na mkutano wa Baraza la
Madiwani Novemba mosi kwa lengo la kufanya uchaguzi huo.
Akizungumza na JAMBO LEO, Diwani wa
Ubungo, Boniface Jacob ambaye pia ni mgombea wa umeya wa Manispaa hiyo, alisema
barua hiyo imefuata sheria na taratibu kwa kutolewa wiki moja kabla ya uchaguzi
huo.
“Kwenye uchaguzi wa awali barua yao
ilieleza kuwa ulikuwa wa dharura jambo ambalo si sahihi. Wametambua makosa yao
na pia ule haukusema kuwa kutakuwa na mkutano wa Baraza la Madiwani,” alisema.
Kuhusu idadi ya madiwani, Jacob alisema
ni lazima waibuke na ushindi, kwa sababu Chadema na CUF kwa pamoja wana idadi
kubwa ya madiwani kuliko CCM.
“CUF ina madiwani wawili, Chadema 10
pamoja na wabunge wawili, CCM wana madiwani wawili. Madiwani wa viti maalumu,
CCM wana mmoja na Chadema watatu. Kwa takwimu hizo tayari tumeshashinda,”
alisema.
“Katika uchaguzi wa awali pia tulikataa
uamuzi wa Mkurugenzi kutaka Mwasa (Salama wa CUF) na Lyimo (Susan wa Chadema)
kupiga kura Ubungo wakati wanaishi Kinondoni.
“Katika uchaguzi huu hatutakubali pia
wajumbe hawa kupiga kura maana wanastahili kushiriki uchaguzi wa Kinondoni,”
alisema.
Alifafanua kwamba kwa kuwa waliokuwa
wagombea wa umeya na naibu meya wa Kinondoni walifungua kesi kupinga matokeo ya
wagombea wa CCM, wana imani Mahakama itatenda haki ili wahusika washiriki
kuchagua meya kihalali.
0 comments:
Post a Comment