Wakili John Malya |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
inajipanga kutoa tarehe rasmi ya kuanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya
umeya wa Kinondoni, ambayo yalimpa ushindi Benjamin Sitta, iliyofunguliwa na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hatua hiyo inakuja baada ya kesi hiyo namba 3 ya
mwaka huu kupangiwa hakimu ambaye ni Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage wa Mahakama
hiyo.
Wakili wa Chadema, John Malya, alisema jana kuwa
walifungua kesi hiyo baada ya juzi kushindwa kufanya hivyo kwa sababu muda wa
kazi ulikuwa umepita, kwa hiyo wanasubiri Mahakama ipange tarehe.
Mbali na Sitta ambaye alipata kura zote 18
walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya George Manyama (CCM),
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa
Manispaa hiyo.
Alisema walifikia uamuzi wa kwenda mahakamani
kutokana na mchezo mchafu waliochezewa na CCM katika uchaguzi huo uliofanyika
Oktoba 23 ukiambatana na kukiukwa kwa sheria na taratibu ambazo zilitakiwa kufuatwa.
Malya alisema wanaiomba Mahakama itengue umeya
wa Sitta, kwa sababu CCM walikaaa wenyewe na kujichagua kutokana na mambo yao
ambayo waliyapanga katika kikao hicho, hali ambayo ilisababisha wao wagomee
kikao hicho.
"Tunaiomba Mahakama iamuru uchaguzi wa Meya
ufanyike mara moja kwa kufuata kanuni, kisije kikatokea kama kilichotokea awali
kwa CCM kupanga matokeo," alisema Malya.
Pia alisema katika hati yao wanaiomba Mahakama
iwaamuru Kagurumjuli na wasimamizi wote wa uchaguzi wafuate taratibu za
kisheria.
Aliongeza kuwa wanaiomba pia Mahakama iwaamuru
wadaiwa walipe gharama za kesi huku akisema pia walalamikaji katika kesi hiyo
ni Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro ambaye pia alikuwa mgombea na
aliyekuwa Naibu Meya Jumanne Mbunju.
Katibu wa Chadema Dar es Salaam, Henry Kileo
alisema walikimbilia mahakamani kwa sababu haki yao iliporwa wazi wazi.
Alisema kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo
kuahirishwa ni kukiukwa taratibu hivyo
Mkurugenzi wa Ubungo na Ofisa Tawala wa Ubungo waliahirisha uchaguzi huo baada
ya kubaini kuna taratibu zilikiukwa kama zilivyokiukwa Kinondoni.
Kileo alisema Kinondoni walitumia ubabe na
kushindwa hata kusikiliza malalamiko ya madiwani, ambao ndio waliwasilisha
malalamiko yao Ubungo wakaahirisha uchaguzi.
Pia alisema Mkurugenzi hana mamlaka ya kuandaa
kikao, kilichofanyika juzi kuchagua Mwenyekiti na si Meya kwa sababu akidi
haikutimia.
"Madiwani wetu walikataliwa kuingia
Manispaa jambo ambalo si haki kabisa, kwa hiyo nawaambia Ukawa wote hatumtambui
Sitta kama Meya, Kinondoni hivi sasa haina Meya. Kama tulivyoanza mitaani,
tukaja mahakamani, tutarudi tena mitaani ili tuendelee kuitafuta haki
yetu," alisema Kileo.
Mbunju alisema kilichofanyika juzi ni mkusanyiko
wa watu walioamua mambo yao kwa kuchaguana, kwa hiyo uchaguzi huo ni haramu.
0 comments:
Post a Comment