Sharifa Marira, Dodoma
LICHA ya wadau wa habari kupinga kwa namna zote Muswada
wa Habari kupelekwa bungeni, Serikali imedhamiria kuupeleka katika Bunge
linaloanza leo ili kusomwa kwa mara ya pili, kuujadili na kuupitisha.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema hayo jana mjini hapa
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba ya shughuli za Bunge
hilo ambalo linaanza leo hadi Novemba 11.
Ndugai alisema pamoja na Muswada huo, pia Serikali
itawasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, ambao pia utasomwa,
kujadiliwa na kupitishwa.
Alisema pamoja na mambo mengine, Bunge litapokea Taarifa
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), ya mwaka 2014/15 na
majibu ya Serikali kuhusu ripoti hiyo.
Miongoni mwa majibu ya Serikali yanayosubiriwa kwa hamu
ni utekelezaji wa maazimio ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
kuhusu ufisadi uliofanyika katika akaunti ya pamoja kati ya Tanesco na Kampuni
ya kufua umeme ya IPTL (Escrow).
Alisema kamati mbili zinazohusu hesabu ambazo ni ya Hesabu
za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitawasilisha taarifa
zao kutokana na vikao vya kamati hizo vilivyofanyika kwa wiki mbili na ripoti
ya CAG ya mwaka 2014/15.
Mambo makubwa ambayo PAC itawasilisha ni suala la mkataba
wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhusu mradi wa ubia baina
yake na Kampuni ya Azimio Housing Estates (AHEL), ambao umeonesha dalili za
shirika kupoteza Sh bilioni 270.
Alisema wabunge watajadili na kushauri Serikali kuhusu makubaliano
ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na Jumuiya
ya Ulaya (AU) na kwamba Bunge linashauri Serikali ndiyo iwe yenye uamuzi wa
mwisho.
Alisema Bunge hilo litakaa kama kamati kwa siku tatu
mfululizo ili kupokea, kujadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuweka
vipaumbele kwenye bajeti ijayo ya Serikali, litapokea taarifa kutoa Kamati ya Sheria
Ndogo.
0 comments:
Post a Comment