Dalila Sharif
JESHI la Polisi Mkoa wa Temeke, linashikilia
vijana 14 wa ‘Panya Road’ na wazazi wao 11, likiwatuhumu wazazi kwa madai ya kukiuka
sheria ya malezi ya watoto wao.
Pia limeonya kuwa kuanzia sasa litawachukulia
hatua kwa kuwashitaki kwa kuficha uovu wa watoto wao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Temeke, Gilles Murato alisema ‘Panya Road’ wanashikiliwa kwa kujihusisha na uvamizi
kwenye Tamasha la Kuinua Vipaji lililoandaliwa na Clouds Fm na kupora wananchi kwa kuwashambulia baadhi
yao na kuwajeruhi.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ya
watoto ya mwaka 2009 vifungu vya 7 na 9 wazazi na walezi wana wajibu wa kulea
watoto wao kwenye mazingira mazuri, ambayo hayatawasababishia madhara
kisaikolojia, udhalilishaji na kuhakikisha wanapata mahitaji ya elimu, afya na
mavazi.
Kutokana na wazazi hao kukiuka sheria
hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya na kwa mujibu wa kifungu cha Sheria
namba 14, mzazi atakayeshindwa kutekeleza
kifungu 7-9 hicho atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atapewa
adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh milioni tano.
"Tunashukuru wananchi wa Buza kwa
kutupa ushirikiano wa kukamata wahalifu hawa, tunaomba waendelee na ushirikiano
huo kwa Polisi ili kukabiliana na vijana hao ambao wamekuwa wakifanya vitendo
viovu dhidi ya raia," alisema Murato.
Wazazi waliofikishwa kituoni hapo,
walisema wanasikitishwa na tabia za vijana wao kujiingiza kwenye makundi ya
kihalifu huku wakisema hawakuwa wakijua kama watoto wao ni ‘Panya Road’.
Enesto Chalo ambaye ni mmoja wa wazazi
hao, alisema alishangazwa kupewa taarifa ya mtoto wake kuuawa kwa kipigo cha
wakazi hao, baada ya wananchi kumgundua kuwa mmoja wa kundi hilo la wahalifu.
"Nimesikitishwa na kitendo cha
mtoto wangu, Issack Ernesto (16) kujiingiza kwenye kundi hilo na kupewa taarifa
kuwa amekufa, lakini alizinduka akiwa mochari," alisema Chalo.
Salumu Ally alisema mtoto wake ni mmoja
wa wanaoshikiliwa kwa uhalifu wa kundi hilo, hivyo alisikitishwa na tabia ya
mtoto huyo kujiingiza kwenye kundi hilo hali nyumbani anaonekana mtiifu.
"Kwa kweli tabia ya kujihusisha na kundi
hili ni hali inayomsababishia mzazi ugonjwa wa moyo kutokana na mwenendo ambao
mtoto huyu anaufanya bila wazazi kujua," alisema Ally.
Watuhumiwa hao walikiri mbele ya waandishi
wa habari kujihusisha na makosa hayo kwa kujiingiza kwenye kundi hilo la ‘Panya
Road’ na kuonesha baadhi ya silaha walizokuwa wanatumia kufanyia matukio ya
kihalifu.
Tukio hili si la kwanza kutokea Temeke
hali inayosababisha baadhi ya wakazi kuishi kwa woga, hivyo Jeshi hilo liliwataka
wakazi hao kushirikiana nalo kutoa
taarifa za uhalifu unaojitokeza.
0 comments:
Post a Comment