Suleiman Msuya
Maalim Seif Sharif Hamad |
KAMATI Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF)
imepitisha ratiba ya ziara za ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa chama kwa kanda
zote itakayoongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho.
Taarifa uliyotolewa jana na Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Mbarala Maharagande ilisema ziara hiyo
itaanza hivi karibuni katika kanda zote saba.
Alizitaja kanda hizo kuwa ni ya Ziwa,
Kati, Pwani, Nyanda za Juu Kusini, Kusini, Kaskazini na Magharibi.
Maharagande alisema Kamati kuu inawataka
viongozi na wanachama kujiandaa kwa wakati.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF wajibu
wa Kamati hiyo ni; “kuhakikisha chama wakati wote kinakwenda na wakati katika uhusiano,
mawasiliano na utendaji wa kisayansi na uyakinifu na kinatekeleza kazi za kila
siku.”
Aidha Kamati hiyo ilipokea na kujadili
hali ya kisiasa na matukio yaliyojitokeza hususan kwa madiwani wa CUF Tanga
kushiriki na au kutoshiriki katika uendeshaji wa shughuli za halmashauri ya
manispaa hiyo na ilichukua suala hilo kwa uzito mkubwa.
Kaimu Naibu Mkurugenzi huyo alisema
Kamati kuu iliagiza suala hilo kushughulikiwa kwa uharaka kwa kuunda kamati ya
kitaifa ya kulisimamia.
“Hivyo Kamati kuu inawataka wanachama wa
CUF Tanga na nchini kwa ujumla, na wapenda mabadiliko kuwa watulivu katika
kipindi hiki ambacho suala hilo linatafutiwa ufumbuzi sahihi na chama,” alisema.
Kamati pia ilitoa pongezi kwa viongozi
wa chama ngazi zote, wanachama, wapenzi wa CUF na wananchi kwa ujumla ambao
wameendelea kuwa madhubuti, kusimamia ajenda muhimu za chama.
Alisema wana CUF na wananchi wako pamoja
na hawakubali kuyumbishwa na watu wachache wenye dhamira ovu ya kutaka kuwatoa kwenye
ajenda muhimu ya kudai haki, usawa na mabadiliko ya kisiasa nchini.
0 comments:
Post a Comment