Peter Kimath, Morogoro
WAZIRI wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza Chuo cha Ardhi mjini hapa
kitumike katika urasimishaji wa makazi, kutokana na kukosa wataalamu wa
kutosha kukamilisha kazi hiyo.
Waziri Lukuvi
alisema jana kuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri wataalamu wa kupima na
kupanga makazi hayo na waliopo hawatoshelezi, hivyo ili kuondokana na makazi
ambayo hayajapimwa ni vema wataalamu wa chuo hicho wakatumika.
Alisema ili
kuchukua muda mfupi ipo haja ya kutumia chuo hicho na kampuni zinazotambulika, zilizosajiliwa na
wizara hiyo kwa upimaji wa ardhi na makazi.
Mkurugenzi wa
Manispaa ya Morogoro, John Mgalula alisema wanatarajia kupata mkopo wa Sh milioni
100 kutoka benki ya CRDB, fedha zinazotarajiwa kurasimisha viwanja 1,000 kwa
majaribio.
Kauli hiyo ya
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ilisababisha Waziri Lukuvi kuitaka Manispaa
kuacha kusubiri mikopo na badala yake itumie mbinu mbadala ya kuzungumza na kampuni
na chuo hicho cha ardhi ili kukubaliana kupima.
Mkuu wa Chuo, Desderius
Kimbe alisema chuo kiko tayari kufanya kazi hizo kutokana na kwamba wana
wataalamu hao ambao wanaweza kufanya kazi hizo, pia wana vitendea kazi vya
kutosha kufanikisha kazi hiyo.
Mratibu wa
Urasimishaji Ardhi, Adolph Milunga alisema mbali na kuwa chuo
pekee kinachofundisha wataalamu wa upimaji ardhi katika ngazi ya Shahada
na Stashahada, chuo hicho pia kinafanya upimaji ardhi na kutoa ushauri juu ya masuala
ya ardhi.
Milunga alishauri
wananchi wa Morogoro, ili kupunguza gharama wajiunge kwenye vikundi katika maeneo yao
badala ya kuomba kupimiwa mmoja mmoja.
0 comments:
Post a Comment