Abraham Ntambara
BAADHI ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamelalamikia huduma
za Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), wakisema
haziridhishi na zimekuwa zikitolewa kwa kusuasua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti la JAMBO LEO
jana, wakazi hao walisema huduma si ya kuridhisha kutokana na kukaa vituoni
muda mrefu wakisubiri usafiri huo.
Saumu Shaibu alisema hali hiyo hujitokeza mara nyingi
asubuhi na jioni watu wakienda kazini na wanafunzi shuleni na jioni wanaporudi
nyumbani.
“Jioni na asubuhi ndiyo kwa kiasi kikubwa tatizo hilo hujitokeza
kwa maana hiyo tunakuwa wengi kwenye vituo na tunakaa kwa muda mrefu huku
magari yakionekana kuwa machache,” alisema Saumu.
Moses James alisema kwa jinsi wanavyokumbwa na adha hiyo
inaonekana kana kwamba magari yamepungua barabarani, kutoa huduma hiyo hali
inayosababisha kuwa machache na hivyo kutoa huduma isiyokidhi mahitaji ya
wasafiri.
“Magari yanaonekana kama yamepungua, ni machache ikilinganishwa
nasi watumiaji wa huduma hii, wakazi wa Dar es Salaam ambao ndio watumiaji kwa
kiasi kikubwa wa huduma,” alisema James.
Aidha, aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wamekuwa
wakijikuta wanavuruga ratiba zao kwa kuwa wanachelewa shughuli zao wakati walikuwa wanaamini usafiri
huu kwa kiasi kikubwa ungewaondolea adha ya upotevu wa muda na kufanya shughuli
zao za kiuchumi.
Halfan Rashid aliongeza kuwa bado tatizo la chenji pia
limeendelea kuwa kero kwa kuwa sehemu za nauli ya Sh 650 wamekuwa wakilipa Sh 700
huku wanapokatisha tiketi za mabasi hayo wakisema hawana Sh 50 za kuwarudishia.
“Kwa kweli hili ni tatizo na tunalilalamikia kwa muda
mrefu wao hawaoni wajibu wa kutafuta hizi chenji, lakini sisi ndio wanatwambia
tuje nazo na kama huna kamili hawarudishi chenji, mbona wao tukiwa na pungufu
hawaturuhusu?” Alihoji Rashid.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba kampuni
hii inajiendesha kwa hasara na ndiyo maana huduma zake zinakuwa za kusuasua.
Ofisa Habari wa UDART, Deus Bugaywa alipoulizwa kuhusu madai ya kampuni kujiendesha
kwa hasara, alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa kuwa halijatolewa na uongozi wa
Kampuni na kubainisha kwamba kila mtu anaweza kuzungumza analojua.
“Nani kasema, taarifa hizo umezitoa wapi? Hebu jaribu
kufanya tathmini tena halafu uulize. Mimi siwezi kuzungumzia hilo kwa kuwa
halijatolewa na uongozi na kila mtu anaweza kuzungumza analojua yeye,” alisema
Buganywa.
Aidha, kuhusu malalamiko ya abiria kuchelewa kwenye vituo
na mabasi kupungua, alisema anavyofahamu ni kwamba kila mtu anajua idadi ya
mabasi yaliyoko barabarani kutoa huduma.
0 comments:
Post a Comment