Celina Mathew
Charles Mwijage |
SERIKALI imetaka Watanzania wanaomiliki
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, washiriki maonesho ya viwanda nchini
yanayotarajiwa kuanza Desemba 7 hadi 11 kwenye viwanja vya maonesho vya Mwalimu
Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Maonesho hayo yenye kaulimbiu ya:
‘Tanzania Sasa Tunajenga viwanda’, lengo lake ni kuwaaminisha wananchi juu ya falsafa na ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuwahamasisha kuthubutu
kujenga viwanda kwa kuwakutanisha walioanza siku nyingi na wapya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema lengo la maonesho
hayo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025, pamoja
na kujenga jukwaa la wadau wa sekta ya viwanda kupata fursa ya kujadiliana,
kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo.
Alisema pia yatatoa fursa za kutoa
taswira ya juhudi za ujenzi wa viwanda kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,
kutangaza bidhaa na huduma zinazotolewa nchini ili kutoa hamasa kwa Watanzania
kutumia bidhaa na huduma za viwanda vya ndani.
Aidha, alisema yataunganisha wenye
viwanda na wazalishaji wa malighafi na huduma zingine za viwandani, kutoa
semina na mijadala ya kitaalamu ikihusu maendeleo ya viwanda nchini, kutangaza
fursa za masoko ya ndani na nje na kuwezesha watafiti na wabunifu kujadiliana
na wenye viwanda juu ya kuboresha teknolojia za uzalishaji na Tehama.
Nyingine ni kuwezesha vijana na
wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira na masomo ya masuala ya viwanda ikiwamo
kuwajengea tamaa ya kuanzisha viwanda,
kutoa fursa kwa wananchi kutambua viwanda vilivyopo na kuwatia hamasa ili
kuwekeza katika viwanda na mamlaka husika zinazotumia maonesho hayo kutangaza
fursa za uwekezaji katika mikoa yote ya Tanzania yakiwamo maeneo ya kujenga
viwanda.
“Kama
mnavyojua mpango wa pili wa miaka mitano unatamka wazi kuwa sekta binafsi ndiyo
mhimili wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo maonesho haya mhusika mkuu ni
sekta binafsi na Serikali ni wawezeshaji,”alisema.
0 comments:
Post a Comment