Grace Gurisha
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya Uhujumu Uchumi,umeieleza
Mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amewaeleza kuwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), bado inaendelea kumchunguza
aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na
wenzake.
Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi
Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,Cyprian Mkeha, baada ya Wakili wa washtakiwa hao
Alex Mgongolwa kulalamika kuchelewa kukamilika kwa upelelezi.
"Upelelezi haujakamilika, lakini DPP ametuambia
Takukuru wanaendelea kuwachunguza washtakiwa, kwa hiyo upelelezi ukikamilika
watasema,"alidai Kishenyi
Akiwasilisha malalamiko hayo, Mgongolwa alidai kuwa ni
miezi sita sasa wateja wake wapo gerezani bila kujua hatua yoyote ya upelelezi
ulipofikia.
"Upande wa Jamhuri unaiingiza Mahakama gizani, kwa
sababu kila kesi inapokuja wanadai upelelezi bado ukizingatia ni miezi sita
sasa mara kwa mara wanaambiwa wanaendelea kufanya upelelezi.
"Kama walijisalimisha wenyewe na wakashtakiwa bila
mabishano yoyote, kwa nini waseme upelelezi bado, kwa hiyo tunaomba watuambia
wamefikia wapi, kwa sababu washtakiwa wanateseka gerezani,"alidai
Mgongolwa
Hakimu alisema shauri hilo limebadilishiwa hakimu
mwingine, ambapo hivi sasa litakuwa kwake, kwa hiyo wahakikishe upelelezi
unakamilika ndani ya wakati ili kesi iendelee na hatua nyingine. Kesi hiyo
imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka huu.
Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni aliyekuwa miss
Tanzania wa mwaka 1996,Shose Sinare na aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo
Arumeru Mashariki Sioi Solomon ambaye pia ni mkwe wa zamani wa Waziri
Mkuu,Edward Lowassa wote ni wafanyakazi wa benki ya Standard.
Mashtaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na
kutakatisha fedha, ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo
halali dola za Marekani milioni 6, sawa na sh bilioni 12.
Awali, upande wa mashtaka uliieleza mahakama katika
tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 Dar es Salaam, washtakiwa hao
watatu walipanga kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa
mahakamani kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu
ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo Kinondoni mshtakiwa, Sinare akiwa
na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ya Agosti
2, 2012. Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walipandishwa kizimbani Aprili Mosi
mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment