Adda Ouko, Musoma
Tundu Lissu |
ALIYEKUWA Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la
Bunda Mjini, Lucy Msoffe ameshindwa kuithibitishia Mahakama kama alipeleka
barua ya kutaarifu wagombea ubunge na vyama vyao, kuhusu kupunguzwa kwa vituo
vya kupigia kura kutoka 199 hadi 190.
Pia, Msoffe ambaye ni shahidi namba
mbili wa upande wa utetezi, hakuthibitisha kuwapo barua ya kuwataka wagombea
kuhudhuria hatua ya kuhesabu kura.
Juzi, kitabu cha kupokelea nyaraka
alichokionesha Wakili Tundu Lissu anayemtetea Mbunge wa Jimbo hilo Esther
Bulaya, hakikuonesha aliyepokea nyaraka hizo.
Msoffe aliiambia Mahakama kuwa alimtuma mhudumu
wa ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Masaulu Oktoba 16, mwaka jana
kupeleka barua yenye orodha ya vituo 190 na kusainiwa na Katibu wa Wilaya wa CCM.
Hata hivyo kitabu cha kupokelea nyaraka
hakikuonesha saini ya Katibu huyo.
Aidha, alidai kuwa hakumbuki siku
alipopeleka orodha ya vituo 199 na mwaliko katika ofisi za vyama vya wagombea
na kusainiwa na makatibu wa wilaya.
Alitoa madai hayo alipohojiwa na wakili
wa waleta maombi, Hajira Mgura aliyemtaka kuionesha Mahakama sehemu iliyotiwa
saini na Katibu huyo kwenye kitabu cha kupokelewa nyaraka.
Akiulizwa maswali na Wakili Hajira,
Msoffe alidai kuwa hakupata barua kutoka ofisi ya CCM ikionesha jina la wakala
wa majumuisho na mgombea.
Shahidi huyo alikiri kwamba kwa mujibu
wa sheria, Msimamizi wa Uchaguzi akikamilisha upokeaji wa matokeo kutoka
vituoni, ndipo huandika barua ya kutaka wagombea au mawakala kufika kwenye
ukumbi wa majumuisho.
Hata hivyo, alikubali kuwa aliandika
barua hiyo kabla ya kumaliza kupokea matokeo kutoka vituoni na haikuwa sahihi.
0 comments:
Post a Comment