Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini na
Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila
amesema amepatwa na mfadhaiko kwa kitendo cha kuahirishwa kwa mahojiano katika
Kituo cha Televisheni cha Clouds kupitia kipindi cha 360.
Kafulila alisema amepatwa na mfadhaiko
mkubwa kwa mahojiano hayo ambayo yalikuwa yanahusu kujadili mambo mbalimbali ya
nchi na kwamba kitendo hicho kina mkono wa viongozi wa Serikali wakubwa.
“Inasikitisha kuona kipindi kimetangazwa
tangu jana (juzi) na nimefika na kuvaa kipaza sauti halafu unaambiwa kuna agizo
kutoka kwa mkurugenzi kipindi kisirushwe nimefadhaika sana sana,” alisema.
“Hadi kipindi cha magazeti saa mbili asubuhi
nilikuwa studio na mtangazaji akatangaza kuwa
baada ya magazeti Kafulila ataingia kujadilia masuala mbalimbali
yanayoendelea nchini.
Nikiwa studio tayari nimevaa kipaza
sauti, ikaombwa radhi kwamba kuna maelekezo kutoka kwa mkurugenzi kuwa kipindi
kisirushwe,” aliongeza
Kafulila alisema anadhani kulikuwa na
maelekezo ya ziada nje ya mfumo wa Clouds Tv kwa sababu haamini kama tangazo
limerushwa kutwa nzima jana (juzi) na jana asubuhi bila mkurugenzi huyo kujua.
Mbunge huyo wa zamani alihoji iwapo
mkurugenzi huyo hakujua bado vipindi ni suala la wataalamu wa utangazaji kuliko
mmiliki na kwamba hajajua hofu yao ilikuwa wapi.
Mkuu huyo wa idara alisema
kinachoondelea kwa sasa kwa mtazamo wake ni kuminya uhuru wa vyombo vya habari,
huku akibainisha kuwa Sheria ya habari inayokwenda kupitishwa bunge lijalo,
vyombo vyote vitakuwa chini ya ulinzi wa dola.
“Binafsi sikutarajia siku moja kukutwa
na hali hiyo sikujua kama siku moja Tanzania itafika hatua hii nilijisikia vibaya
kuvuliwa kipaza sauti nikiwa tayari kwa mjadala, lakini nilijua tatizo ni zaidi
ya watangazaji,” alisema.
Aidha, alisema alikuwa amejipanga
kuelezea tatizo la mwenendo wa uchumi kuanzia namna Serikali iliyorithi uchumi
mbovu na haionekani kutambua hilo na kujizatiti na badala yake hali imezidi
kuwa mbaya.
Alisema pia alitaka kuzungumzia kwa
mapana anguko la sekta ya fedha na sekta binafsi na mazingira ya biashara na
uwekezaji kwa ujumla na namna athari yake inavojitokeza kwenye kupunguza uwezo
wa serikali kutoa huduma kama elimu, afya,
kwa mujibu wa repoti mbalimbali za tafiti.
“Nilitaka kuhitimisha kwa kuzungumzia
mwenendo wa vita ya ufisadi, hatua zinazochukuliwa na maoni juu ya nini bado hakijafanyika,”
alisema.
Aidha, kwa upande mwingine Chama cha
NCCR-Mageuzi kimetoa taarifa ya kulani kitendo cha Kafulila kutofanya mahojiano
hayo na kuwataka Watanzania kutambua kuwa kuna kazi kubwa ya kulinda demokrasia
na utawala wa sheria.
0 comments:
Post a Comment