Grace Gurisha
David Mataka |
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege
la Tanzania (ATCL), David Mataka, amedaiwa kumwandikia barua aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Grey Mgonja aidhinishe maombi ya kukodisha ndege bila kufuata
sheria ya ununuzi, hali ambayo iliisababishia Serikali hasara ya dola
772,402.08 za Marekani.
Hayo yalidaiwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu mstaafu
wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga, baada ya
Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali
na kukiri kumwandikia barua Mgonja.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Mlinga alikiri kuwa
Februari 27, 2008 Mgonja alimwandikia barua kutaka kujua kama mchakato wa
kukodisha ndege unaofanywa na ATCL unafuata sheria za ununuzi, akamjibu Mgonja
kuwa hawafuati utaratibu huo.
Ilidaiwa kuwa Machi 12, 2008 Mlinga alimwandikia
Mataka kumshauri kuwa amwandikie Mgonja ili apate idhini ya makubaliano na
Serikali ya kukodisha ndege bila kufuata sheria hiyo.
Machi 19, 2008 Mataka aliomba idhini hiyo kwa
Mgonja, na kusababisha Mgonja naye aandike barua kwa Mlinga ili kupata ushauri,
ambapo siku hiyo hiyo naye aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Idara ya
Uthibitisho wa Mali za Umma wakutane kuzungumza suala hilo.
Vitalis alidai kuwa tarehe hiyo hiyo, Mlinga
alimshauri Mgonja kuidhinisha mchakato huo, kwa sababu tayari kulikuwa na
makubaliano yaliyokwishafanyika baina ya ATCL na kampuni ya Wallis Trading Inc
ya Liberia.
Mataka alikanusha madai yote yalikuwa
yakimkabili ya kuisababishia Serikali hasara ya dola hizo, lakini akakiri taarifa
zake binafsi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 23 ambapo
mashahidi wa upande wa mashitaka
watasikilizwa. Mbali na Mlinga na Mataka, mshitakiwa mwingine ni mwanasheria wa
PPRA, Bertha Soka.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita
yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuisababishia hasara
Serikali kupitia ukodishaji wa ndege.
Wakili Vitalis alidai kuwa Oktoba 9, 2007
katika ofisi za ATCL wilayani Ilala, Mataka alitumia vibaya madaraka kwa kusaini
mkataba wa ukodishaji ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 baina ya
Wallis Trading Inc na ATCL.
Alidai alifanya hivyo bila kuzingatia Sheria ya
Ununuzi wa Umma na taratibu za zabuni kwenye mchakato huo.
Pia, alidai kuwa Oktoba 27, 2007 alitumia
vibaya madaraka yake kwa kusaini cheti cha kuruhusu mchakato wa ukodishaji ndege
hiyo bila ya kufuata ushauri wa kiufundi na kuisababishia Serikali hasara ya
dola 772,402.08 za Marekani zilizolipwa kwa kampuni ya Aeromantenimiento, S. A
kama gharama za huduma ya matengenezo.
0 comments:
Post a Comment