* Kaya zaidi ya 450 zahaha mahali pa kuishi
* Mbomoaji asema
ni wavamizi wasio na haki
Dotto Mwaibale
Baadhi ya wakazi wa Madale |
KAYA zaidi ya
450 hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao zaidi ya 150 kubomolewa Tegeta
A, kata ya Goba, Dar es Salaam kwa madai ya kujengwa eneo lisilo lao.
Ubomoaji huo,
ulifanyika jana ukisimamiwa na askari wa Jeshi la Polisi chini ya kampuni ya
Udali ya Yono Aution Mart, ambao hata hivyo umepingwa na wananchi hao wakidai
eneo hilo ni lao na wapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Ubomoaji wa
nyumba hizo ulisimamiwa na polisi zaidi ya 15 wenye silaha za moto na mabomu ya
machozi huku wakiwa katika magari matatu.
Mmoja wa
wananchi waliobomolewa nyumba zao, Macarios Turuka aliiambia JAMBO LEO kwamba
eneo hilo kwa kipindi kirefu lilikuwa halitumiki na lilikuwa vichaka vya
wahalifu ambapo wanawake walikuwa wakibakwa na kutumiwa na watu kwa uhalifu
ndipo walipoingia na kujenga.
Aliongeza kuwa
baada ya kuanza ujenzi, aliibuka mtu ajulikanaye kwa jina la Benjamin Mutagwaba
akidai ni lake, ndipo walipofungua kesi Mahakama ya Kimara ambako alishindwa
kupeleka vielelezo vya umiliki wa eneo hilo.
Mwanasheria
anayetetea wananchi hao, Moses Chunga alisema kitendo cha kubomoa nyumba hizo
ni ukiukaji sheria, kwani kuna kesi ya msingi namba 188/2016 waliyofungua Mahakama
Kuu ya Ardhi ambapo walitakiwa Oktoba 31 waende kuisikiliza, lakini walishangaa
kuona nyumba hizo zikibomolewa.
Alisema wananchi
hao wanajipanga kudai fidia ya uharibifu huo na kuwa kabla ya yote wanahitaji
kumwona Rais wapate haki yao.
Mkurugenzi wa
Yono Auction Mart, Yono Kevela alisema kampuni yake imevunja nyumba hizo kwa
amri ya Mahakama na polisi walikuwapo kusimamia.
"Mwenye
eneo hilo ambaye ni Kanisa la Winers alishinda kesi mwaka mmoja uliopita na leo
(jana) ulikuwa ni utekelezaji wa kuondoa wavamizi," alisema Kevela.
Mkazi wa eneo
hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamisi alisema kitendo walichofanyiwa
si cha kiungwana kwani wao wapo eneo hilo kwa
siku nyingi hata
kufikia hatua ya kujenga nyumba hizo, mmiliki
huyo alikuwa wapi kwa siku zote hizo.
"Kwa kweli
hawa watu wanatufanya tusiipende Serikali yetu tunaomwomba Rais atusaidie
katika jambo hili," alisema Hamisi.
Hamisi alisema leo
wanatarajia kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kupeleka kilio chao na kama
akishindwa watakwenda kwa Mkuu wa Mkoa na kama
napo hawatapata
ufumbuzi watakwenda kumwona Waziri William Lukuvi na Rais.
Hawa Musa
alisema baada ya kuvunjiwa nyumba zao wapo katika wakati mgumu na hawajui
wataishije na watoto wao.
Alisema
wamepanga vitu vyao nje na mvua yote iliyonyesha jana ililowanisha vyombo vyao
yakiwamo magodoro na hawajui huyo mtu anayedai ni eneo lake nyuma yake kuna
nani.
"Tangu
tufungue kesi Mahakama ya Kimara hakuwahi kufika, kama yupo kweli kwa nini
anashindwa kuhudhuria mahakamani?" Alihoji Musa.
Musa aliongeza
kuwa kabla ya kubomoa nyumba hizo walipaswa kutoa notisi, lakini hawakufanya
hivyo walifika saa mbili asubuhi na kubomoa bila hata ya
kushirikisha viongozi
wa eneo hilo.
Mkazi mwingine,
Juma Abdallah alilalamikia polisi kuchukua televisheni, kisimbuzi na Sh 80,000 ndani.
"TV yangu
na kisimbuzi na Sh 80,000 zimechukuliwa," alilalamika Abdallah.
Katika hatua
nyingine wananchi hao walimtupia lawama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa
Tegeta A, kuwa amekuwa akikumbatia watu wanaodai kuwa eneo hilo ni
lao, wakati anaelewa fika ukweli halisi.
Mwenyekiti huyo,
Marko Vaginga alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari
kuzungumza chochote zaidi ya kumtaka mwandishi kwenda ofisini
kwake.
"Nakuomba
uje ofisini tuzungumze, kwa leo siko tayari kuzungumza chochote," alisema
Vaginga na kukata simu.
0 comments:
Post a Comment