Fidelis Butahe
MBUNGE wa Makete (CCM), Profesa Norman
Sigalla amesema ameijulisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kuhusu sakata la kuingiziwa kiasi cha Sh.
milioni 5 katika akaunti yake ya benki, akisema hajui aliyeidhinisha alipwe.
Amesema kuanzia Januari hadi Aprili
mwaka huu, aliingiziwa Sh. milioni 1.2 katika akaunti hiyo na kwamba haziwezi kuwa za mshahara wa ukuu
wa Wilaya ya Songea kwa sababu aliacha wadhifa huo tangu Julai mwaka jana,
baada ya kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kugombea ubunge wa
Makete na kushinda.
Sigalla alitoa kauli hiyo jana katika
kipindi cha Power breakfast kinachorushwa na Redio Clouds Fm, baada ya kudaiwa
kupokea mshahara wa ukuu wa wilaya wa miezi mitano wakati akiwa mbunge.
“…Nikavijulisha vyombo vya usalama kama
Takukuru, watizame huyu anayeingiza fedha anaingiza kwa nia gani, kwanini
ahuishe akaunti ya mkuu wa wilaya ambayo imefungwa, kwanini haingizi hizo fedha
zote, zingine zinakwenda kwa nani?” alihoji.
“Nilipomaliza ukuu wa wilaya akaunti
yangu ilisimamishwa na hakuna fedha nilizolipwa. Sasa iweje baada ya miezi sita
kupita ndio nianze kuingiziwa fedha.”
Katika ufafanuzi wake Sigalla alisema, Juni
mwaka huu aliandikiwa barua na Katibu wa Bunge, akielezwa kuwa amepokea barua
kutoka kwa Katibu Tawala mkoa wa Ruvuma, ikieleza kuwa mbunge huyo alikuwa akipokea
mishahara miwili, ya ubunge na ukuu wa wilaya.
“Akaunti hii ambayo mshahara wa ukuu wa
wilaya ulikuwa ukipitia kwa sasa ndio ninayopitishiwa mshahara wa ubunge…,nilipopewa
ile barua nilihamaki na nilichofanya ni kukimbilia benki kuchapisha bank
statement (taarifa binafsi za kibenki), kuanzia siku niliyoacha ukuu wa wilaya
hadi mwezi Juni nilipopewa barua hiyo,” alisema.
“Nilipoitazama sikuona mshahara wa Sh
milioni 4.6 ukiingia…, baadaye tulikwenda mbali zaidi…, tuligundua kuwa kuna Sh
milioni 1.2 imeingia kuanzia Januari hadi Aprili na fedha hiyo haionyeshi inaingizwa na nani zaidi ya kusomeka salary
transaction.”
Alipoulizwa sababu za kutobaini
kuingizwa kiwango hicho cha fedha, alisema haikuwa rahisi kwake kubaini hilo.
“Agosti mwaka huu nilimwandikia
barua Katibu wa Bunge na kumtajia
kiwango cha fedha kilichoingia katika akaunti yangu (Sh milioni 5) na kumwomba
kikatwe katika mshahara wangu wa ubunge au malupulupu na kirudishwe Hazina,”
alisema.
“Nikasema anayeingiza (fedha hizo) achukuliwe
hatua ili aeleze ameingiza kwa nia gani, pili akaunti hii ilikuwa haiingizi
fedha zozote za mkuu wa wilaya, sasa iweje imefufuka na kuingiza kiasi hicho
cha fedha, ni kitu gani, maana huo si mshahara wa mkuu wa wilaya.”
Alisema ili mtu aweze kufungua akaunti iliyofungwa
anahitaji kuwa na nywira na kusisitiza mtu huyo ni rahisi kumbaini.
“Hii si bahati mbaya. Ingekuwa baada ya
kuacha ukuu wa wilaya na fedha kuendelea kuingia tungesema ni bahati mbaya,
lakini ilishafungwa kwa miezi sita, sasa unapoifungua si bahati mbaya, je
ulitumwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment