Mkanganyiko waahirisha kesi ya Lwakatare, mwenzake


Grace Gurisha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imelazimika kuahirisha kesi ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare na mwenzake, baada ya kutokea mkanganyiko kutokana na upande wa Jamhuri kudaiwa kula njama za kutokujua jalada halisi la kesi hiyo liliko.

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita alijikuta jana kwenye wakati mgumu baada ya kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kutajwa, kwa sababu walikata rufaa kupinga dhamana ya washitakiwa, kwa hiyo jalada halisi la kesi liko Mahakama ya Rufaa.

Hali hiyo ilimshitua Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba ndipo akalazimika kumwuliza Lwakatare kama anajua chochote kuhusu hilo, akasema suala hilo ni jipya, kwa sababu rufaa ya kesi iliyo mbele yake ni vitu viwili tofauti.

Hakimu alimwunga mkono Lwakatare kuwa rufaa hiyo haihusiani na kesi hiyo na pia jalada halisi la kesi liko mahakamani na ndilo analotumia, kwa hiyo hajui wakili wa Serikali anazungumzia jalada lipi.

Kutokana na hali hiyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 17 itakapotajwa na kuangalia hatua ya kesi ilikofikia.

“Naombeni mfuatilie mjue kesi hii imefikia hatua gani, kwa sababu hata nikikuuliza swali lolote hapa huwezi kunijibu, hujui lolote. Fuatilieni, vinginevyo kesi haitakwisha, tangu mwaka 2013 hadi leo kesi haijaisha,” alisema Hakimu Simba.

Mbali na Lwakatare mshitakiwa mwingine ni Joseph Ludovick, ambao wanakabiliwa na madai ya kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.

Machi 20, 2014, Lwakatare na wenzake walifunguliwa rasmi kesi namba 6/2013 ya tuhuma za ugaidi, ambapo tuhuma za pili, tatu na nne hazina dhamana na hivyo Mei 8, mwaka jana, Jaji Lawrence Kaduri alifuta mashitaka hayo, kwa maelezo kuwa hakuona  maelezo ya kutosha kuwafungulia mashitaka ya aina hiyo.

Baada ya kufutwa mashitaka hayo, walibaki na ya kula njama, ambayo yana dhamana, kwa hiyo wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya Mahakama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo