Suleiman Msuya
CHAMA cha Wananchi (CUF), kinatarajiwa
kuwasilisha mahakamani maombi yake ya kutengua uamuzi wa Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini wa kumrejesha Profesa Ibrahim Lipumba kwenye uenyekiti wa chama
hicho.
CUF pia inatarajia kuiomba Mahakama kumwonya
Msajili asiwe anaingilia uamuzi wa chama hicho na vingine.
Mwanasheria wa CUF, Hashim Mziray jana
aliiambia JAMBO LEO Dar es Salaam, kwamba kila kitu kinachohusika na maombi
hayo kimekamilika hivyo matarajio yao ni kuwa leo watawasilisha ili Mahakama
iweze kufanyia kazi.
Mziray alisema wahusika wote ambao
walipaswa kusaini ombi hilo wameshasaini na kuwa ni jukumu la jopo la
wanasheria kuwasilisha ili haki iweze kutendeka.
“Kila kitu kiko tayari nadhani leo
tutawasilisha maombi yetu mawili ambayo yatakuwa na vipengele vingine vidogo
ila msingi mkubwa ni kuiomba Mahakama iondoe agizo la Msajili kwa CUF,”
alisema.
Alisema katika kesi hiyo, watakaoshitakiwa
ni Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali George Masaju, Lipumba, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Thomas Malima
na wengine ambao wamekuwa katika mgogoro na chama.
Mwishoni mwa wiki, JAMBO LEO ilipozungumza
na Kambaya ambaye yuko upande wa Lipumba, alisema wanasubiri kitakachotokea
mahakamani ila kwa sasa hakuna hatua wanayochukua.
Aidha, kwa upande mwingine, Mjumbe wa
Kamati ya Uongozi wa Chama hicho Katani Katani, alisema wamepita maeneo yote
ambayo Lipumba amepita katika ziara yake na kugundua kuwa hakuna madhara yoyote
ambayo ameacha.
Katani alisema baada ya kupita na
kuzungumza na wanachama asilimia kubwa walionesha kutoelewa chanzo cha mgogoro,
hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha.
”Tumezunguka katika Wilaya ya Newala,
Mtwara Mjini, Nachingwea, Masasi na maeneo mengine kimsingi hakuna madhara
yoyote jambo la kusikitisha ni pale ambapo unapowaambia wafuasi wa Lipumba
tupitie Katiba ya chama hawana hoja wanakimbia,” alisema
Alisema asilimia kubwa ya kundi la
Lipumba wamekuwa wakisimamia hoja ya kutaka busara itumike na si Katiba ya
chama, hivyo kuonekana dhahiri kuwa wameshindwa.
0 comments:
Post a Comment