Suleiman Msuya
KAMATI Kuu ya Utendaji Taifa Chama cha
Wananchi (CUF) imepitisha ratiba ya ziara za ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa
chama kwa kanda zote itakayoongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho.
Taarifa uliyotolewa na Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF, Mbaraka Maharagande ilisema ziara hiyo
itaanza hivi karibuni kwa kuzifikia kanda zote nchini ikiwemo Kanda ya ziwa,
Kati, Pwani, Nyanda za Juu Kusini, Kusini, Kaskazini na Magharibi.
Maharagande alisema kamati kuu inawataka
viongozi na wanachama kujiandaa na ziara hizo na kuhakikisha maandalizi yote ya
msingi yanakamilika kwa wakati.
“Kamati kuu imepitisha ratiba ya ziara za
ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa chama kwa kanda zote kwani hilo ni moja ya
lengo la chama cha siasa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF
Ibara 85(1) na (3) ni wajibu wa kamati ya utendaji Taifa; “kuhakikisha kuwa
Chama wakati wote kinakwenda na wakati katika mahusiano, mawasiliano na
utendaji wa shughuli za Chama kisayansi na uyakinifu” na “kinatekeleza kazi za
kila siku za chama ngazi ya Taifa” aliongeza.
Aidha kamati hiyo imepokea na kujadili
hali ya kisiasa na matukio yaliyojitokeza kuhusiana na madiwani wa CUF katika
jiji la Tanga kushiriki na au kutoshiriki katika uendeshaji wa shughuli za halmashauri
ya manispaa hiyo na kwamba imelichukua suala hilo kwa uzito mkubwa.
Kaimu Naibu Mkurugenzi huyo alisema
kamati kuu imeagiza suala hilo kushughulikiwa kwa uharaka kwa kuunda kamati ya
kitaifa ya kulisimamia suala hilo.
“Hivyo kamati kuu inawataka wanachama wa
CUF Tanga na nchini kwa ujumla, na wapenda mabadiliko kuwa watulivu katika kipindi
hiki ambacho suala hilo linatafutiwa ufumbuzi sahihi na chama,” alisema.
Kwa upande mwingine kamati hiyo imetoa
pongezi kwa viongozi wa chama kwa ngazi zote, wanachama, wapenzi wa CUF na
wananchi wote kwa ujumla ambao wameendelea kuwa madhubuti, imara zaidi
kusimamia ajenda muhimu za chama hicho.
Alisema hadi sasa wana CUF na wananchi
wapo pamoja na hawakubali kuyumbishwa na watu wachache wenye dhamira ovu ya kutaka
kuwatoa katika ajenda muhimu ya kudai haki, usawa na mabadiliko ya kisiasa nchini.
Maharagandec alisema kamati kuu
imesisitiza kuwa CUF ipo imara na itaendea kuweka mipango madhubuti ya
kujiimarisha ndani ya chama na kujenga ushirikiano makini na vyama rafiki katika
UKAWA.
Aidha alisema kamati kuu inazipongeza taasisi
za Kimataifa ambazo mara zote zimekuwa na msaada mkubwa kuwezesha ufanikishaji wa
programu mbalimbali za chama ikiwemo utoaji mafunzo kwa viongozi na wanachama.
0 comments:
Post a Comment