Salha Mohamed
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeichukua Benki ya Twiga na
kusitisha huduma zake kwa wiki moja, baada ya kupungua mtaji na kuhatarisha usalama
wa sekta ya fedha na amana za wateja.
Uamuzi huo wa BoT ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa
chini ya kifungu cha Sheria namba 56(1)(g)(i) na 56(2)(a)-(d) ya mabenki na
taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema jana kuwa kupungua
kwa mtaji huo ni kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki.
“Benki Kuu ya Tanzania imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi
na uongozi wa Benki ya Twiga na kumteua Meneja Usimamizi atakayekuwa na jukumu
la kusimamia shughuli za Benki ya Twiga kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya
usimamizi wa BoT,” alisema.
Alisema utoaji wa huduma za benki hiyo utasitishwa kwa wiki
moja ili kutoa nafasi ya kupanga shughuli za uendeshaji wa benki hiyo.
Profesa Ndulu aliongeza kuwa BoT haina haja ya kuisimamia
benki hiyo kwa kipindi chote, kama atatokea mwekezaji anayeweza kuimiliki.
Alisema benki hiyo iliyokuwa chini ya Serikali kwa
asilimia 100, mwaka juzi iliongeza mtaji baada ya BoT kuitaka kufanya hivyo,
lakini bado hali haikuwa nzuri kutokana na madeni kuwa mengi na
yasiyokusanyika.
0 comments:
Post a Comment