*Aombwa
ajielekeze Escrow, Lugumi
Fidelis
Butahe
Rais John Magufuli |
SIKU kama ya leo mwaka mmoja uliopita,
Watanzania walikuwa wakisubiri kwa hamu matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyomweka
madarakani Rais John Magufuli ambaye katika kipindi cha takribani mwaka mmoja
wa uongozi wake, anatajwa kukata mirija 10 ya ulaji, JAMBO LEO linachambua.
Rais huyo wa Awamu ya Tano ambaye aliapishwa
Novemba 5 mwaka jana, amekuwa akieleza mikakati yake, ikiwamo ya kubana
matumizi ambayo baadhi ya wananchi wanaieleza kusababisha ‘kukausha’ fedha
mifukoni na kwamba sasa hali ni ngumu zaidi.
Wakati ubanaji huo wa matumizi ukigeuka kilio
kwa baadhi ya wananchi ambao Rais amekuwa akisisitiza wafanye kazi ili kuzipata
kwa sababu za bure bure hazipo kwenye utawala wake, hali imekuwa tete zaidi kwa
wapiga dili na waliotumia mgongo wa Serikali kujipatia fedha kinyume na
taratibu.
Wachambuzi waliozungumza na JAMBO LEO mbali na
kupongeza hatua zilizochukuliwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi katika kipindi
chake kifupi cha utawala, wakimtaka kushughulikia vigogo ‘wapiga dili’ lakini walitaja
kasoro waliyoibaini kuwa ni ya kuminya demokrasia.
Walitaja baadhi ya maeneo ambayo Dk Magufuli
hajayagusa na vigogo wanatajwa kuhusika ni; mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi
Enterprises inayodaiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, wizi wa fedha kutoka akaunti
ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) na mgawo wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo, mirija iliyozibwa
na Rais Magufuli tangu aingie madarakani ni; malipo ya watumishi hewa, mapato
ya taasisi za udhibiti kwenda mfuko mkuu wa Serikali, kuzuia taasisi na idara
za Serikali kufanya mikutano na makongamano nje ya kumbi zao, kuziba mianya ya
rushwa bandarini na uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na kufuta sherehe
mbalimbali za kitaifa.
Nyingine ni kiinua mgongo cha wabunge kukatwa
kodi, maduka binafsi kuondolewa katika hospitali za serikali, kufuta safari za
nje na kuondoa utaratibu wa kuuzia askari na wanajeshi bidhaa zisizolipiwa kodi
kupitia maduka maalumu kwenye kambi za majeshi.
Maoni
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Benson Bana alisema: “Amerejesha imani ya Serikali kwa wananchi maana awali
tulikuwa tunajiuliza kuna Serikali au hakuna…, ameonesha kuwa mfumo mzuri wa
uongozi kwenye taasisi hauwezi kutosha bila usimamizi na ufuatiliaji
unaoeleweka.
“Hatua zake za kubana ubadhirifu bandarini na
kuishukia Wizara ya Fedha na Mipango, zilikuwa na maana. Ila katika hili la
kubana demokrasia watu lazima waelewe kuwa demokrasia lazima iambatane na utii
na uwajibikaji.”
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha
Ruaha aliungana na Dk Bana, lakini akipinga kuhusu demokrasia kwa maelezo kuwa,
uamuzi wa Rais kuzuia mikutano ya kisiasa ni sawa na kuzuia Watanzania kujua
jinsi nchi yao inavyotafunwa.
Alisema wapinzani nao wana nafasi kubwa ya
kufichua maovu na ulaji unaofanywa na wachache serikalini, na kumwomba Rais alitafakari
upya katazo hilo.
“Ukitazama EPA, Escrow na hata Lugumi, ni kashfa
ambazo kwa kiasi kikubwa ziliibuliwa na wapinzani na nyingine ni katika
mikutano ya hadhara,” alisema.
“Rais amebana matumizi, amerejesha uwajibikaji,
amepambana na watumishi hewa, ufisadi na rushwa, ingawa bado naliona tatizo
katika kushughulikia vigogo waliohusika katika kashfa mbalimbali, mfano ni ile
ya Escrow.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema utawala wake wa mwaka mmoja umeonesha
mafanikio katika baadhi ya mambo, licha ya kuwa hajabana vigogo sawasawa.
“Haina maana kama anatatua changamoto ndogo
anaacha mambo makubwa kama Lugumi na Escrow… tunataka ayashughulikie ili
tuamini kuwa ana dhamira ya kutukomboa,” alisema.
Alisema Rais anapaswa kuongeza juhudi katika
sekta za elimu na afya ambazo bado zina changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.
Alibainisha kuwa Rais anatakiwa kutambua kuwa
mafanikio yoyote yanahitaji ushirikiano wa pande zote na si kwa mfumo wa
ubaguzi ambao unasababisha malalamiko.
Mbunge Viti Maalumu CUF, Salma Mwasa alisema jitihada za Rais tangu
aingie madarakani hazijatoa mwelekeo kwa wananchi, hivyo anapaswa kujitathmini
upya.
Alisema hali ya maisha ya wananchi ni ngumu isiyoendana
na hatua alizochukua tangu aingie madarakani.
“Unaona jinsi Rais na wasaidizi wake
wanavyotumia Jeshi la Polisi kuminya demokrasia, kimsingi uamuzi huo unapunguza
uaminifu kwa wananchi licha ya kupenda matamshi kuwa anapenda Watanzania wote,”
alisema Mwasa.
Watumishi
hewa
Katika sherehe za Mei mosi zilizofanyika kitaifa
Dodoma, Rais Magufuli alisema mpaka wakati huo watumishi hewa walikuwa 10,295 kwa mwezi wakilipwa Sh bilioni 11.63, na
kutoa mfano kuwa kama fedha hizo zingetumika katika maendeleo zingejenga
madaraja matatu kama la Nyerere la Kigamboni, barabara za juu saba kama
zinazojengwa Dar es Salaam.
Huenda fedha hizo zilikuwa zikitafunwa na
wachache kabla ya kubainika.
Sherehe
Mbali na agizo lake la kutaka viongozi wa
Serikali walioalikwa kwenye kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kurejesha posho
walizopewa, Novemba 8 mwaka jana, ikiwa ni siku tatu baada ya kuapishwa, Rais alitangaza
kuokoa Sh milioni 225 zilizochangwa kugharimia hafla ya wabunge na kuagiza
zinunulie vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Pia alifuta sherehe za Uhuru za Desemba 9 mwaka
jana na kuamuru Sh bilioni 4 zilizokuwa zitumike, zipelekwe kupanua barabara ya
Morocco-Mwenge.
Pia alifuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi na
kuagiza fedha zilizopangwa kutumika, zikanunulie dawa za kupunguza makali ya
Ukimwi (ARV).
Rais pia aliahirisha sherehe za Muungano Aprili
26 na kuokoa Sh bilioni 2 na kutaka zitumike kupanua barabara ya Ghana hadi
Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Safari
Novemba 7 mwaka jana, Rais alitangaza kufuta
safari za nje ya nchi hadi uamuzi mwingine utakapotolewa. Alisema shughuli zote
zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaowakilisha
Tanzania nchi za nje na watakaosafiri ni kwa vibali maalumu.
Uamuzi huo ulionekana kuziba mianya ya baadhi
ya viongozi kujipatia fedha zilizokuwa zikitengwa kwa ajili ya safari.
Mikutano
Katika hotuba yake bungeni Novemba 20, mwaka
jana Rais alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi, zikiwamo za warsha,
semina, makongamano na matamasha kufanyika katika kumbi za taasisi za Serikali
au wizara.
Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa ilisababisha baadhi
ya hoteli kupoteza wateja wa uhakika, ambao ni taasisi za Serikali.
Bandari
Mara baada ya kuchaguliwa, Rais Magufuli mara
kwa mara amekuwa akifanya ziara kwenye bandari ya Dar es Salaam, sambamba na kuwachukulia
hatua watendaji waliobainika kuwa na tuhuma, zikiwamo za kutafuna mabilioni ya
fedha.
Mpaka sasa takriban watumishi 50 wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Bandari Tanzania (TPA) wamefukuzwa kazi.
Usafirishaji
Mbali ya hatua alizochukulia watendaji wa Shirika
la Ndege Tanzania (ATCL) na wa viwanja vya ndege nchini kutokana na tuhuma,
hivi karibuni aliagiza kufanyika uchunguzi wa gharama za upanuzi wa uwanja wa
ndege wa JNIA, baada ya kubaini upanuzi wake kugharimu zaidi ya Sh bilioni 7.
Wabunge
Uamuzi wa Rais kutaka kiinua mgongo chake
kukatwa kodi sambamba na kutaja mshahara wake wa Sh milioni 9.5, ulikuwa mwanzo
wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutangaza mpango wa Serikali
katika bajeti ya mwaka 2016/17, kukata
kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge, ambao awali walikuwa hawakatwi.
Maduka
Mkakati wa Wizara ya Afya kukomesha wizi wa
dawa unaofanywa na watumishi wasio waaminifu kwa kuandaa mkakati wa kuondoa maduka
binafsi ya dawa kwenye hospitali za Serikali, lilikuwa ni pigo lingine
lililobana ulaji wa baadhi ya watu na watendaji wa Serikali wasio waaminifu.
Mapato
Ulaji mwingine uliobanwa baada ya Serikali
mwaka 2016/17 kuamua mapato ya taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Maji na Mafuta (Ewura), Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi
(Trafiki) na mamlaka nyingine za udhibiti, kupelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko
Mkuu wa Serikali ambako mahitaji ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na
Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa na mapato yaliyokusanywa.
Majeshi
Katika mwaka 2016/17 wa fedha, maduka ya kutoa
huduma kwa askari yalifutiwa kodi na badala yake Serikali inajipanga kuongeza
posho kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na
ofisi zote za Serikali, zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni
asiyetumia mashine za kukusanyia kodi (EFD).
0 comments:
Post a Comment